Yohane Gervas, Rombo
LICHA ya juhudi mbalimbali zinazoendelea kufanywa na Serikali katika Wilaya ya Rombo, mkoani Kilimanjaro za kuzuia ulevi muda wa kazi pamoja na usambazaji na uuzaji wa pombe haramu ya gongo bado imeonekana suala hilo kushika kasi katika maeneo mbalimbali katika wilaya hiyo.
Serikali wilayani humo ilipiga marufuku mtu kunywa au kuuza pombe muda wa kazi, yaa ni kuanzia majira ya asubuhi hadi saa kumi kwa siku za kazi na kuanzia saa nane kwa siku za mapumziko ya wiki, huku ikizuia kabisa usambazaji na uuzaji wa pombe aina ya gongo. Serikali iliweka zuio hilo kufuatia vitendo vya ulevi kukithiri katika Wilaya ya Rombo, hali iliyochangia kupungua kwa nguvu kazi na kusababisha umasikini miongoni mwa jamii.
Hata hivyo Serikali ilitoa elimu juu ya athari za unywaji wa gongo na ulevi wa pombe kupitia maeneo mbalimbali ikiwemo katika nyumba za ibada. Hata hivyo agizo hilo limeonekana kupuuzwa na baadhi ya wananchi na wafanyabiashara ambapo wanaendelea kuuza na kunywa pombe muda wa kazi.
Baadhi ya wananchi wa Wilaya ya Rombo wakizungumza na mtandao huu wamesema kuwa hali hiyo inachangiwa na vijana wengi kukosa kazi na hivyo kuamua kulewa muda wote na pia wamesema kuwa tatizo hilo limnachangiwa na baadhi ya viongozi kushindwa kusimamia sheria zilizowekwa.
Mkuu wa Wilaya ya Rombo, Elinasi Pallengyo alikiri kuwepo kwa tatizo hilo hivi karibuni alipokuwa akizungumza katika kikao cha Baraza la Madiwani na kwenye maadhimisho ya siku ya sheria nchini ambapo alisema kuwa operesheni hiyo ilikuwa imesitishwa kidogo katika kipindi cha sikukuu za mwisho wa mwaka na lakini akasisitiza kuwa operesheni hiyo kwa sasa inaendelea ili kuhakikisha sifa ya ulevi katika wilaya hiyo inaisha.
“…Tulikuwa tumesitisha kidogo operesheni hiyo kwa sababu ya sikuku za mwisho wa mwaka likini sasa tunaendelea na hatutalala,” alisema Pallengyo.
Aidha aliwataka madiwani pamoja na wadau wengine wakiwemo waandishi wa habari kutumia nafasi zao kutoa elimu juu ya madhara ya ulevi ili kuhakikisha wananchi wanaondokna na tatizo hilo.