Na Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
WIZARA ya Biashara, Viwanda na Masoko kupitia Shirika la ZSTC imesema tayari imenunua jumla ya tani 4,466.03 za karafuu kwa thamani ya milioni 66,990.5 kutoka kwa wakulima, hadi kufikia Januari 23, 2012 na bado zoezi hilo linaendelea ikiwa ni wastani wa tani 10 hadi 18 kwa siku.
Uongozi wa Wizara ya Biashara, Viwanda na Masoko chini ya Waziri Nassor Ahmed Mazrui, ulitoa taarifa hiyo kwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Muhamed Shein, Ikulu mjini Zanzibar alipokutana na timu hiyo.
Mkutano huo ni muendelezo wa kukutana na Wizara za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika kuangalia Mpango Kazi wa utekelezaji wa Bajeti ya mwaka 2011/2012 kwa kipindi cha robo ya kwanza na ya pili ya mwaka.
Uongozi wa Wizara hiyo ulieleza kuwa kati ya karafuu zote zilizouzwa na Shirika, mauzo ya tani 1,500 kwa dola 17,900,000 milioni ambazo ni sawa na Shilingi za Kitanzania bilioni 27,670,421,934 yameshafanyika katika kipindi cha mwezi wa Januari 2012.
Aidha, uongozi huo ulieleza kuwa ili kusimamia hali ya mwenendo wa jumla wa bei kwa bidhaa muhimu hasa chakula serikali ilichukua hatua za kisoko ambnazo zilizihusisha kufanya mashauriano na wafanyabiashara kuandaa kanuni mpya na taratibu za biashara.
Kutokana na maelezo ya Wizara chini ya utaratibu huu mpya bei za bidhaa hasa chakula sasa zinapangwa kwa kushirikiana baina ya Serikali na Wafanyabiashara wenyewe kwa ujumla, utaratibu huu umejitokeza kufanya kazi vizuri na bei za chakula kuwa na mwenendo mzuri.
Ukitolea mfano bei ya chakula, uongozi huo ulieleza kuwa bei ya sukari iliopo sasa hapa Zanzibar sh. 1900 kwa kilo wakati bei ya bidhaa hiyo kwa nchi nyengine za Afrika Mashariki ni wastani wa sh. 2,500-3,000 kwa kilo moja.
Pia, uongozi huo ulieleza kuwa Wizara imekamilisha utafiti wa kutathmini uwezekano wa kuifanya Zanzibar kuwa eneo tengefu (SEZ) la kiuchumi ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki. Sambamba na hayo uongozi huo ulitoa pongezi kwa Dk. Shein na kueleza kuwa uongozi wake thabiti ndio uliopelekea mafanikio hayo makubwa.
Nae Dk. Shein alitoa pongezi kwa uongozi wote wa Wizara hiyo pamoja na watendaji wake likiwemoa Shirika la ZSTC na Kikosi Kazi kwa juhudi zao za kuhakikisha zao la karafuu linaimarika sanjari na wananchi kushajiika kuuza karafuu zao serikali.
Aidha, Dk. Shein pia, alitoa pongezi kwa wananchi wote wa Unguja na Pemba kwa mashirikiano yao ikiwa ni pamoja na kuuza karafuu zao serikalini na kusisitiza kuwa ule wasiwasi uliokuweko kwa baadhi ya watu kuwa hali hiyo haitowezekana kuwa imewezekana tena kwa mafanikio makubwa. Pia, Dk. Shein alieleza haja ya kuwekwa mikakati zaidi katika uimarishaji wa sekta ya viwanda.
Dk. Shein pia, alisisitiza kuwa kuna ulazimu wa kuwasaidia wakulima hasa wa viungo kutokana na umuhimu wa mazao hayo sanjari na soko lake lilivyoimarika hivi sasa hasa pilipili, mdalasini, hiliki, manjano na mengineyo.
Wakati huo huo, Dk. Shein alikutana na uongozi wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali chini ya Waziri wake Mhe. Ramadhan Abdalla Shaaban kwa madhumuni hayo hayo na kupongeza juhudi za Wizara hiyo katika kuimarisha sekta ya elimu.
Dk. Shein alieleza kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imejiwekea mipango kabambe ya kuiimarisha sekta hiyo ya elimu ikiwa ni pamoja na kukiimarisha Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) ili kiweze kufundisha kada ya Udaktari hapo baadae.
Akisoma taarifa ya utekelezaji wa kazi za Wizara hiyo, Waziri Shaaban alieleza kuwa kazi za ukarabati wa skuli za sekondari za Fidel Castro na Utaani zinaendelea na zinatarajiwa kukamilika katika mwezi Julai mwaka huu kama ilivyopangwa. Pia alisema kuwa ukarabati wa skuli ya Forodhani na Tumekuja unaendele.
Aidha, alieleza kuwa taratibu za kuwapata wakandarasi kwa ajili ya kazi za ujenzi wa Skuli tano kubwa za sekondari katika maeneo ya Kiembesamaki, Mpendae, Kwamtipura, Kibuteni na Mkanyageni zinaendelea na tayari kwa upande wa skuli ya Mpendae mkandarasi ameshapatikana na wakati wowote ujenzi utaanza
Sambamba na hayo, uongozi huo wa Wizara ya Elimu ulieleza mikakati iliyoweka katika juhudi zake za utoaji mikopo kwa wanafunzi huku ikieleza pia mikakati iliyowekwa kwa wale wote waliopata mikopo hiyo siku za nyuma na wameshamaliza masomo kufanya taratibu za kuirejesha ili na wenzao wafaidike.