Na Mwandishi Wetu
WAKATI zoezi la uandikishaji wapigakura likianza leo maeneo mbalimbali ya jijini Dar es Salaam tayari yameanza kujitokeza mapungufu kwa baadhi ya waandikishaji kukosa umakini hasa wa uandikaji majina katika mfumo huo, huku pia kukiwa na baadhi ya watu ambao sio raia wakijitokeza kutaka kujiandikisha, jambo ambalo huenda likasababisha kuandikishwa kwa watu wasiostahili katika zoezi hilo.
Mfano katika kituo cha Shule ya Msingi Mapambano ‘B’ waandikishaji wa moja ya Chumba wameonekana kukosa umakini na kazi wanayoifanya pasipo na sababu huku wakiwa wagumu hata kukubali kuwa wanamakosa. Katika kituo hicho mmoja wa wananchi aliyefika kujiandikisha alijikuta jina lake linakosewa zaidi ya mara moja huku mwandikishaji akigoma hata kusahihishwa makosa ya jina alilokosea.
Mwandikishaji huyo kwa Mara ya kwanza alipokea fomu ya mteja wake iliyoandikwa jina kwa herufi kubwa jina la FREDY ANTHONY NJEJE lakini yeye aliandika kimakosa jambo ambalo lilimfanya arudie kuchapisha kadi nyingine, baada ya muandikishwaji kuona jina lake linakosewa alimshauri aangalizie kwenye fomu aliyoijaza ambapo mwandishi huyo alikaidi jambo ambalo lilimfanya akosee tena.
“…mwandikishaji kwa kujifanya mjuaji alikaidi kuangalizia kwenye fomu niliojaza, ambapo alipo andika jina kwa mara ya pili akawa amekosea tena baada ya kuandika Fredy A Njeje yeye akaandika Fredy A. Njnje na kujiona ameweza…baadae alipo ulizwa mbona amekosea tena na ni kosa lake, akajibu hawezi kuprint tena hivyo mwananchi angoje mpaka daftari la maboresho, jambo ambalo kimsingi linamnyima mwananchi huyo kujitambulisha kwa kadi hiyo iliyokosewa jina,” alisema mwananchi huyo.
Baadaye mwandikishaji huyo alisema kadi zote zimekosewa hivyo mwandikishwaji achague moja wapo achukue, la sivyo asubiri mpaka daftari la maboresho wakati mwananchi huyo alishakaa zaidi ya saa nane akingoja kujiandikisha. Hata hivyo mwananchi huyo alilazimika kuondoka huku hajui kama atapata haki ya kupiga kura au lah kutokana na majina yake kukosewa.
Pamoja na hali hiyo, katika kituo hicho cha Mapambano ‘B’ walijitokeza watu wawili ambao walionekana sio raia wa Tanzania kwani baada ya kuhojiwa walikuwa hawajui sehemu walipozaliwa nchini Tanzania, hawamfahamu hata Rais wa Tanzania, Dk. Jakaya Kikwete na hawamfahamu pia Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere na hata wimbo wa Taifa hawaujui.
Baada ya watu hao kushtukiwa waliondoka kinyemela bila kuchukuliwa hatua yoyote. Kituo hicho pia hakikuwa na chombo chochote cha usalama kama Polisi ili kuangalia usalama wa Raia wanaojiandikisha, jambo ambalo lilitoa fursa kwa wazamiaji. “Hii ni siku ya kwanza tu, safari bado ndefu tuna siku tisa Mbeleni, Swali la kujiuliza Je Hawa waandikishaji walipewa mafunzo na kuyaelewa? Pili je kuachiwa kwa watu wanaodhaniwa kuwa sio Raia wa Tanzania hii ni Sawa.”
Taarifa ambazo mwandishi wa habari hizi amezipata pia katika kituo cha Shule ya Msingi Bangulo Kata ya Pugu Stesheni, watuwaliojitokeza asubuhi walikuwa zaidi ya 1000 moja huku kikiwa na mwandikishaji mmoja mwenye mashine moja, hadi kufikia saa saba na nusu mwandikishaji alikuwa amewaandikisha raia 73 na baada ya hapo wino ulimwishia huku akiwa na orodha nje ya takribani raia 1181 ambao walikuwa kwenye orodha kusubiri kuandikishwa.
“…Kituoni kwetu Bangulo Kata ya Pugu Shtesheni idadi ya watu ni wengi sana zaidi ya elfu moja na mwandikishaji yupo mmoja akiwa na mashine moja tu…na amesikika akisema mashine yake ina uwezo wa kuandikisha watu 50, sijui wengine itakuwaje,” alisema Joram Kinanda mkazi wa Pugu Stesheni.
Hali ya idadi kubwa ya wananchi huku uwezo wa mashine na watendaji kupungua ilionekana pia katika Kituo cha Shule ya Msingi Tabata na Vituo vya jirani pia huku kukiwa hakuna ulinzi wa askari katika vituo vingine.