Zitunzeni Kadi za Kupigia kura Msibadilishe na Chochote


Na Anna Nkinda – Maelezo, Lindi

Wakazi wa mkoa wa Lindi wametakiwa kuzitunza shahada zao za kupigia kura na kukataa kurubuniwa ili waziuze kwani kadi hizo ndizo zitazowawezesha kupiga kura na kuwachagua viongozi wanaowataka.

Mwito huo umetolewa hivi karibuni na Mke wa Rais Mama Salma Kikwete wakati akiongea kwa nyakati tofauti na wananchi wa vijiji vya Nyengedi na Mandawa vilivyopo katika majimbo ya Mtama na Ruangwa waliohudhuria mkutano wa kampeni ya kuwanadi wagombea wa nafasi za udiwani, ubunge na urais kupitia tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Mama Kikwete ambaye ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM kupitia wilaya ya Lindi mjini alisema kadi ya mpiga kura ndiyo itakayomuwezesha mwananchi aliyejiandikisha kumchagua kiongozi anayemtaka siku ya uchaguzi ikifika.

“Ikitokea mtu anakuja kwako na kukwambia nitakupa mkopo wa shilingi 30,000/= au 50,000/= nipe kadi yako ya kupigia kura usikubali! ukimpa tu utakuwa umepoteza haki yako ya msingi ya kupiga kura kwani hatakurudishia hadi uchaguzi utakapoisha”, alisisitiza Mama Kikwete.

MNEC huyo pia aliwasihi wanawake kutoogopa siku ya uchaguzi ikifika wajitokeze kwa wingi kupiga kura kwani kutakuwa na usalama wa kutosha, ulinzi utaimarika na uchaguzi utaenda vizuri kama ilivyopangwa.

Mama Kikwete aliwaomba wananchi hao kutopoteza kura zao bali wafanye maamuzi sahihi na kuwachagua viongozi kutoka CCM ambao wamewaletea na wataendelea kuwaletea maendeleo endelevu kwa kuwa chama hicho kina kuna Ilani ilani ya uchaguzi inayoeleweka ambayo ni mkataba baina ya CCM na wananchi.

Kwa upande wake mgombea ubunge kutoka jimbo la Mtama Nape Nnauye alisema ushindi kwa CCM uko wazi na kuwataka wanamtama kutembea kifua mbele kwani Serikali imefanya mambo mengi ikiwemo kuimarisha huduma za afya, elimu, barabara, umeme na maji.

Nape alisema, “Changamoto iliyopo hapa ni kutokuwa na daraja katika mto Lukuledi kwani wananchi wanne wamepoteza maisha wakati wakivuka kwenda kulima ng’ambo ya pili mkinichagua nitahakikisha daraja linajengwa kwani kazi ya Serikali ni kutengeneza mazingira mazuri ili wananchi wake waweze kujipatia riziki”.

Nape ambaye ni Katibu Uwenezi na Itikadi wa CCM alisema katika eneo hilo kuna umeme lakini umewekwa katika nyumba chache wakati wananchi wameshafanya wire ring katika nyumba zao na kuona kuwa kuna uzembe unafanyika na kuahidi kulifanyika kazi suala hilo.

Naye mgombea ubunge wa jimbo la Ruangwa Majaliwa Kassim Majaliwa aliwaomba wananchi wa jimbo hili kumchagua tena kwa kipindi cha miaka mitano ijayo kwani katika kipindi chake cha Ubunge kilichopita kazi aliyoifanya wameiona anataka afanye tena kazi ya kuwatumikia wananchi ili waweze kushirikiana kuleta maendeleo zaidi.

Majaliwa alisema, “Hivi sasa katika jimbo letu tuna walimu wa kutosha, maji yapo, barabara zipo kwa mfano barabara ya Mandawa – Milola haikuwa inapitika kirahisi sasa inapitika, minara wa mawasiliano ipo na bado inaendelea kujengwa katika maeneo ambayo hakuna, umeme nguzo zinaendelea kusambazwa nawaomba tuzidi kushirikiana ili turekebishea mapungufu yaliyopo”.

Majaliwa ambaye ni Naibu waziri ofisi ya waziri mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Alisema wananchi wa eneo hilo wanakabiliwa na upungufu wa chakula kutokana na kutopata mvua za kutosha kipindi cha kilimo kilichopita na kumuomba Mama Kikwete aweze kuwasaidia ili wananchi hao wapate msaada wa chakula.

Katika mkutano wa hadhara uliofanyika kijiji cha Mandawa jumla ya wanachama 34 walihamia CCM ambapo wanachama 22 walitoka Chama cha Wananchi (CUF) na 12 chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).

Mama Kikwete aliweka jiwe la msingi katika ofisi ya CCM kata ya Mandawa na kuwaahidi wanachama wa chama hicho kuwapatia shilingi milioni moja kwa ajili ya kununua mabati ya kuezekea jengo hilo.