Na Shomari Binda wa Binda News-Musoma
WADAU wa Habari wametakiwa kuzitumia ofisi za kamati za maadili za vilabu vya Habari vya Mikoa katika kusuluhisha migogoro baina ya vyombo vya habari na wadau wa Habari zinazo jitokeza katika utendaji wa kazi.
Hayo yamesemwa Mjini Musoma katika mafunzo ya maadili yaliyotolewa na Meneja wa maadili na usuluhishi kutoka Baraza la Habari Tanzania (MCT) Allan Lawa, wakati akitoa mafunzo katika ofisi za Chama cha Waandishi wa Habari Mkoani Mara (MRPC) zilizoko katika Jengo la Bodi ya Pamba.
Alisema kuwa lengo la (MCT) kukutana na kamati za maadili za vilabu vya Waandishi wa Habari Mikoani ni kutaka kutatua matatizo ya Wananchi wanaoumizwa na waandishi wa habari sambamba na wadau wanaowaumiza waandishi wa habari .
Lawa alisema Wadau wanapaswa kuleta malalamiko yao katika ofisi ya klabu ya Waandishi wa Mkoa wa Mara (MRPC) katika usuluhishi ambapo pia utaimarisha ueledi wa Waandishi wa Habari utakaongeza uajibikaji wa Waandishi wa Habari na utajenga imani ya watumia Habari.
Alisema kuwa Baraza la Habari Tanzania ni chombo pekee nje ya mahakama ambacho kinavisadia vilabu katika kuvijengea uwezo wa kusuluhisha migogoro hivyo Wananchi wanaochafuliwa na vyombo vya Habari ikiwemo Redio,Televisheni na Magazeti ni vyema wakaleta malalamiko katika ofisi za (MRPC) tayari kwa kusikilizwa kabla ya shauri kulipelekwa Mahakamani.
Alisema lalamiko lililoko mahakamani halipaswi kusikilizwa na kamati na kufanya hivyo ni kuidharau mahakama hivyo ni bora kluanzia kwanza katika kamati ya maadili.
Kamati ya maadili itapitisha maamuzi kwa njia ya makubaliano na mlalamikiwa ataombwa kurudisha gharama za kushughulikia tatizo na kuombwa radhi na Gazeti husika ,Tv au Redio na (MCT) na hilo lisipofanyika italifuatilia.
Aidha Lawa alikemea Waandishi wa Habari wanaofedhehesha taaluma ya Habari kuadhibiwa na kamati ya maadili sambamba na Waandishi wasio wanachama wa (MRPC) wakikaidi kuja mbele ya kamati pale watakapokosea.
Alishauri pia kamati ya maadili iundwe na wajumbe mchanganyiko wakiwemo wasio Waandishi wa Habari akiwemo Mwenyekiti lakini awe mkereketwa wa habari,rafiki wa Habari au kiongozi wa Dini alisema Lawa
Lawa aliomba sekretarieti ya (MRPC) ianze kupokea malalamiko ya usuluhishi kuanzia sasa ili kuwasaidia Wananchi wanaoumia au wanaoteseka kwani Waandishi wa Habari wanadhamana kubwa ya kuifikisha mbali tasnia ya Habari na hatimaye kuheshimiwa na jamii.