Zitto Ziarani Kikazi Nchini Ujerumani

Waziri Kivuli wa Fedha na Uchumi, Naibu Kiongozi wa Upinzani Bungeni na Mbunge wa Kigoma Kaskazini ndugu Zitto Zuberi Kabwe

WAZIRI Kivuli wa Fedha na Uchumi, Naibu Kiongozi wa Upinzani Bungeni na Mbunge wa Kigoma Kaskazini ndugu Zitto Zuberi Kabwe ameanza ziara ya kikazi nchini Ujerumani ambapo atahudhuria na kuhutubia Mkutano mkubwa wa masuala ya ushirikiano wa kiuchumi kati ya Ujerumani na Africa. Mkutano huo “Economic Conference: Commitment to Africa Initiative” utafanyika Jijini Berlin kuanzia tarehe 9 – 11 Desemba 2012 na umeandaliwa na Wizara ya Ushirikiano wa Kimaendeleo ya Serikali ya Ujerumani.

Katika ufunguzi wa Mkutano huo ndugu Zitto atatoa mada kuhusu mgongano wa maslahi kati ya Kampuni binafsi na Jamii ambapo ataongelea suala zima la makampuni makubwa ya kimataifa yanavyonyonya rasilimali za Afrika bila kuwajibika kulipa kodi na kuendeleza jamii zinazozunguka shughuli zao. Atazungumzia pia mitaji kiduchu inayokuja Afrika na fedha nyingi inayotoroshwa Afrika kupitia rushwa, ukwepaji kodi na wizi wa rasilimali. Afrika inapoteza zaidi ya dola za kimarekani 583 bilioni kila mwaka kutokana na utoroshaji wa fedha unaofanywa na makampuni ya kimataifa kwa kushirikiana na baadhi ya viongozi wa Afrika. Hata hivyo Afrika inapokea takribani dola za Kimarekani 80 bilioni tu kwa mwaka kutokana na Uwekezaji (FDI) na Misaada (foreign Aid). Tanzania ni moja ya nchi inayopokea misaada mingi kutoka nje na moja ya nchi ambayo rasilimali zake zinatoroshwa na baadhi ya viongozi wake kutorosha fedha na kuzihifadhi kwenye mabenki ya Ulaya kama Uswiss.

Mnamo tarehe 11 Desemba ndugu Zitto atakuwa kwenye jukwaa moja na Waziri wa Maendeleo wa Ujerumani kuzungumzia namna bora ya kushirikiana kati ya Ujerumani na nchi za Kiafrika. Miongoni mwa mapendekezo ya Zitto ni kuondokana na mfumo wa sasa wa ushirikiano wa misaada na badala yake kuwe na ushirikiano wa kujengeana uwezo ili kila nchi iweze kuhimili maendeleo yake yenyewe.

Katika ziara hii Zitto atakutana na Mawaziri Wakuu wa majimbo ya Nord Rhein Westphalen jimbo ambalo limefanikiwa sana katika vita dhidi ya ukwepaji kodi unaotokana na raia wa Ujerumani kuficha fedha kwenye mabenki ya Uswiss na wa jimbo la Lower Saxony kwa ajili ya mazungumzo kuhusu ukarabati wa Meli ya Liemba na kujenga mahusiano kati ya Mkoa huu na Mkoa wa Kigoma pia kati ya mji wa PapenBurg na Manispaa ya Kigoma.

Zitto anatarajiwa kutembelea baadhi ya nchi nyingine za Ulaya na kukutana na watu mbalimbali katika kuimarisha mtandao wa kimataifa dhidi ya utoroshaji wa fedha kutoka Afrika (illicit money transfer). Pia atakutana na watu binafsi wenye ujuzi na weledi katika masuala haya ya kupambana na watoroshaji wa fedha. Zitto anataraji kurudi nchini mnamo tarehe 16 Desemba 2012. Kwa namna itaakavyowezekana umma utapewa taarifa kuhusu ziara hii kupitia akaunti ya twitter na facebook ya ndugu Zitto. Pia mada zote atakazowasilisha zitawekwa kwenye blogu ya zittokabwe.com kila itakapowezekana.

Waziri Kivuli wa Fedha na Naibu Kiongozi wa Upinzani Bungeni anawatakia Watanzania wote kila la kheri katika Sikukuu ya Uhuru wa Tanzania Bara. Utu, Uzalendo, Uadilifu na Uwajibikaji ni silaha muhimu sana za kujenga Taifa lenye heshima na jamii ya watu wenye fursa za kuendeleza maisha yao kwa haki na amani. Tutimize wajibu wetu katika kuijenga Tanzania tuitakayo kwa ajili yetu na kwa ajili ya vizazi vijavyo.

Tarifa hii imetolewa na Ofisi ya Mbunge wa Kigoma Kaskazini
8 Desemba 2012, Dar es Salaam