Zitto, Mnyika wafichua upotoshaji bajeti ya Mkulo

WAZIRI wa Fedha na Uchumi, Mustafa Mkulo, anadaiwa kulipotosha taifa kitakwimu na kimaudhui uliofanywa kwa lengo la kuwajengea wananchi matumaini hewa yenye kuonyesha serikali inawajali na kusikiliza matatizo yao.

Matumaini hayo aliyaonyesha kupitia hotuba yake ya bajeti ya mwaka 2011/2012 juzi ambayo ilionyesha kuwa kutakuwa na nafuu ya maisha wakati hali halisi haipo hivyo.

Kauli hiyo ilitolewa jana mjini hapa na Waziri Kivuli wa Fedha na Uchumi wa kambi ya upinzani, Zitto Kabwe, na Waziri Kivuli wa Nishati na Madini, John Mnyika.

Katika taarifa yao iliyotolewa kwa niaba ya kambi ya upinzani, wabunge hao walisema wameshtushwa na upotoshaji huo ambao walisema una lengo la kuwapa wananchi matumaini hewa.

“Hotuba ya bajeti ya serikali kwa mwaka 2011/2012 ina upotoshaji mkubwa, tuna uhakika ulifanywa kwa makusudi ili kuonyesha serikali inajali matatizo ya wananchi.”

Akiainisha maeneo aliyodai yamepotoshwa, Zitto alisema wakati waziri akitaja kipaumbele cha kwanza cha bajeti hiyo kuwa ni kumaliza tatizo la umeme na serikali imetenga sh trilioni 537, upembuzi uliofanywa na kambi ya upinzani kwenye vitabu vya bajeti (Kitabu Namba II na IV) vilivyotolewa na serikali yenyewe, umebaini kuwa Wizara ya Nishati na Madini imetengewa sh 402,402,071,000 kwa mujibu wa fungu la 58.

Alisema fedha hizo zimegawanywa katika mafungu ya matumizi kawaida sh 76,953,934,000 na kwa upande wa bajeti ya maendeleo zimetengwa sh 325,448,137,000.

Alisema sh bilioni 325 zilizotengwa katika bajeti ya maendeleo ya Wizara ya Nishati na Madini zinatosha kwa mradi mmoja tu wa umeme wa megawati 160 zikiwamo megawati 100 za Dar es Salaam) na 60 za Mwanza.

“Hakuna mradi wowote mpya wa umeme unaoonekana katika bajeti. Ni dhahiri kuwa kauli ya Mkulo ililenga zaidi kuwajengea wananchi matumaini hewa kuliko kuchukua hatua za kweli za kumaliza tatizo la umeme,” ilisema taarifa hiyo.

Eneo lingine la upotoshaji ni hili: wakati waziri na serikali anataka kuwaaminisha Watanzania kuwa bajeti ya mwaka huu imeongezeka kuliko ilivyokuwa ya mwaka 2010/2011, kambi ya upinzani inasema kuwa hakuna ongezeko lililofanyika.

“Bajeti iliyopita ilikuwa sh trilioni 11.6 wakati mwaka huu wa 2011/2012 serikali ina bajeti ya jumla ya sh trilioni 13.525…Kati ya fedha hizo za mwaka huu kiasi cha sh trilioni 1.901 ambazo ni sawa na asilimia 14.06 ya bajeti yote, kitatumika kulipia deni la taifa.

“Kwa mantiki hiyo, mtaona kuwa fedha kwa ajili ya kuendesha serikali pamoja na kugharamia miradi mbalimbali ya maendeleo zitabaki kuwa ni kiasi cha sh trilioni 11.624 ambazo ni sawa na fedha za bajeti ya mwaka wa fedha uliomalizika (Japo thamani ya shilingi imeanguka ukilinganisha na hali ilivyokuwa mwaka 2010/2011).”

Kutokana na hali hiyo, kambi ya upinzani imesema hii si bajeti ya maendeleo bali ni ya madeni.

Katika eneo la tatu la upotoshaji, kambi ya upinzani ilisema wakati waziri akisema bajeti ya mwaka huu itapunguza posho kama sehemu ya mkakati wa serikali wa kuthibiti matumizi, ukweli ni kuwa bajeti hiyo imetenga sh trilioni 2.987, sawa na asilimia 13 ya bajeti yote kwa ajili ya kulipa posho chini ya vifungu vinavyojulikana kama “Personnel allowances (non discretionary na In-kind”).

“Kwa hiyo, kauli ya Waziri Mkulo kuwa serikali itapunguza posho sio kweli. Tunautaka umma wa Watanzania usikubali kurubuniwa,” ilisema taarifa hiyo.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, bajeti ya mwaka huu imewaongezea mzigo mkubwa sana wananchi na haswa wajasiriamali wadogo na vijana ambao wamejiajiri ama kuajiriwa kwenye biashara ya usafiri na usafirishaji.

“Tunasema hivyo, kwa sababu serikali katika bajeti vipaumbele vyake rasmi vya
bajeti ni kufanya marekebisho ya sheria ya usalama barabarani sura 168 ili kuongeza ukomo wa kiwango cha faini inayotozwa kwa kufanya makosa wakati mtu akiwa anaendesha gari yaani (Traffic Notification Fee), kutoka shilingi 20,000 hadi shilingi 300,000.

Lakini Waziri Mkulo katika hotuba yake aliyoitoa jana ukurasa 74, alitamka kuwa wataongeza kiwango cha faini hadi kufikia shilingi 50,000. Ni dhahiri kuwa kauli ya waziri ya kusema faini itafikia 50,000 wakati kwenye vitabu rasmi vya bajeti faini hiyo inaonekana itafikia 300,000, hivyo alilenga kuuhadaa umma na kuupotosha,” alisema.

Taarifa hiyo ilisema kambi ya upinzani imeshtushwa na kushangazwa na hatua ya serikali kutenga zaidi ya robo ya bajeti kulipa madeni na kulipana posho (Asilimia 27 – 14 kulipa madeni na 13 kulipa posho mbalimbali).

Kambi ya upinzani inajipanga kuwasilisha bungeni bajeti mbadala Juni 15, ambayo Zitto alitamba kwamba, itakuwa inajali maslahi ya Watanzania yenye lengo la kukuza uchumi wa vijijini na itajikita katika kupata vyanzo vipya vya mapato na kubana matumizi ikiwemo kufuta posho mbalimbali.

Juzi wakati Waziri wa Fedha na Uchumi, Mustafa Mkulo, akisoma mapendekezo ya bajeti ya serikali kwa kipindi cha mwaka wa fedha wa 2011/2012, aliliambia Bunge kwamba anapendekeza nyongeza ya kiwango cha faini kwa makosa ya usalama barabarani kutoka sh 20,000 za sasa hadi sh 50,000.

Lakini katika hotuba yake iliyochapishwa kwenye vitabu maalum na kusambazwa kwa wabunge, wanahabari na makundi mengine, ilisomeka kuwa amependekeza kiwango cha sh 300,000 badala ya sh 20,000.

“Mheshimiwa Spika napendekeza kufanya marekebisho ya Sheria ya Usalama
Barabarani 168 ili kuongeza ukomo wa kiwango cha faini inayotozwa kwa kufanya makosa wakati wa uendeshaji gari barabarani (Traffic Notification Fee) kutoka shilingi 20,000 hadi sh 300,000,” ilisomeka sehemu ya hotuba ya Waziri Mkulo.

Akizungumzia utata huo, Spika wa Bunge, Anne Makinda, alikiri kuwapo kwa mkanganyiko na kuahidi kuwa Waziri Mkulo atapeleka marekebisho ya usahihi wa faini hiyo.

“Kuna makosa, nadhani waziri ataleta marekebisho ya usahihi wa faini ya makosa ya barabarani,” alisema Spika Makinda.

Wakati Makinda akitoa kauli hiyo, Naibu Spika, Job Ndugai, alisema kwa sasa Bunge linatambua kile kilichoingia kwenye Hansard za Bunge kwamba ndio sahihi.

“Waziri Mkulo alitamka kwamba faini ni sh 50,000. Kwa mujibu wa kanuni za Bunge, hiki kitaingia kwenye kumbukumbu zetu. Kile kiasi cha sh 300,000, hatutakitambua hata kama kimo kwenye vitabu rasmi vya serikali.”

source: freemedia