Zitto Kutoa ya Moyoni Kesho, Awaita Waandishi wa Habari Kuzungumza Dar

Zitto Kabwe

Zitto Kabwe

MBUNGE wa Kigoma Kaskazini kupitia tiketi ya CHADEMA na Naibu Kiongozi wa Kambi Rasmi Bungeni, Zitto Kabwe kesho anatarajia kuzungumza na waandishi wa habari kuzungumzia hatua ya Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo iliofanya uamuzi wa kumvua nafasi zote za uongozi ndani ya chama hicho.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Mbunge huyo jijini Dar es Salaam leo, Zitto anatarajia kuzungumza na wahariri na waandishi wa habari kutoa tamko mara baada ya adhabu aliyopewa ndani ya chama chake. Hata hivyo taarifa ya mbunge huyo haijaweka wazi itazungumzia nini. Pamoja na hayo wachambuzi wa masuala ya siasa wanasema mbunge huyo anatarajia kujitetea juu ya uamuzi uliofanywa na chama chake wa kumvua madaraka yeye pamoja na Mjumbe wa Kamati Kuu wa chama hicho, Dk. Kitilla Mkumbo na Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Arusha, Samson Mwigamba.

“Taarifa inatolewa kuwa Mheshimiwa Zitto Kabwe pamoja na Dk Kitila Mkumbo watakutana na wahariri na waandishi wa habari kesho siku ya Jumapili tarehe 24 Novemba 2013. Watatumia nafasi hii kutoa maoni na msimamo wao kuhusu maamuzi ya Kamati Kuu ya CHADEMA ya hivi karibuni. Mkutano huu na waandishi wa habari utafanyika katika Hoteli ya Serena Jijini Dar es Salaam kuanzia saa5.00 asubuhi,” imesema sehemu ya taarifa hiyo.

Wachambuzi wa masuala ya siasa wanasema kauli ambayo anataka kuitoa mwanasiasa huyo huenda ikawa ya hasira hivyo kutokuwa na msimamo sahihi juu ya mustakabali wake kisiasa kutokana na jazba aliyonayo kwa sasa ikiwa ni siku moja baada ya kuvuliwa nafasi anuai za uongozi ndani ya chadema.

“…Zitto hakupaswa kuzungumza kwa sasa juu ya kilichotokea dhidi yake, bado ni mapema sana huenda atakachokizungumza ikawa ni kauli ya hasira ambayo inaweza isiwe na msimamo halisi juu ya mstakabali wake kisiasa. Kitendo kilichotokea kinamuumiza sana kisiasa kwa sasa lakini hakupaswa kuzungumza mapema,” alisema mmoja wa wachambuzi wa masuala ya siasa akizungumza na mtandao huu.

Zitto ambaye ni mwanasiasa kijana aliyejizolea umaarufu mkubwa nchini Tanzania hapo nyuma amewahi kutoa kauli lilizostua wengi mara kadhaa ikiwemo ya kutaka kuacha siasa na kwenda kufundisha (chuo) ili hali bado anaonekana kukubalika, kugombea urais kupitia chama chake huku wengi wakimpinga ndani ya chama chake; yeye pamoja na Dk. Mkumbo na Mwigamba wamevuliwa uongozi ndani ya chama hicho baada ya kutuhumiwa kuandaa waraka wa siri ambao umekwenda kinyume cha katiba ya chama chao.