Zitto Kabwe Asema Serikali ya JPM Inamawaziri Hewa…!

Kiongozi wa Chama cha ACT Wazalendo, Kabwe Zuberi Zitto (Mb).

Kiongozi wa Chama cha ACT Wazalendo, Kabwe Zuberi Zitto (Mb).

KIONGOZI wa Chama cha ACT Wazalendo, Kabwe Zuberi Zitto (Mb) amesema mawaziri wa Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais John Pombe Magufuli hawana mamlaka ya uwaziri kuweza kufanya kazi kwa kile kutokuwa na ‘Instruments’ jambo ambalo linawafanya kuwa mawaziri hewa.

Zitto ametoa kauli hiyo leo jijini Dar es Salaam alipokuwa akiwahutubia wajumbe wa Mkutano wa Halmashauri Kuu ya Chama cha ACT Wazalendo. Alisema kimsingi kwa sasa Rais anaonekana ni Waziri wa Wizara zote nchini.

“…Hivi sasa Serikali ina mawaziri hewa na hata maamuzi yao ni hewa. Instruments ni jambo la kisheria. Ndio zinatoa mamlaka kwa Mawaziri kufanya kazi. Hivyo kutokana na kutokuwa na Instruments kimsingi Rais ni Waziri wa Wizara zote nchini hivi sasa,” alisema Zitto katika hotuba hiyo.

Aliongeza kuwa; “Natoa wito kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali ahakikishe Mawaziri wanapewa instruments ili waweze kuwepo kisheria na maamuzi yao yawe ya kisheria. Chama chetu kisikubali nchi kuendeshwa na mtu mmoja kwa jina la Rais. Nchi yetu inaendeshwe kikatiba.”

“…Suala la ‘instruments’ ni suala linaloendana na suala la matumizi kubadilishwa. Kimsingi bila instruments Baraza la Mawaziri lina watu 2 tu – Rais na Makamu wa Rais. Kama Waziri Mkuu hana instruments hakuna Waziri Mkuu. Kama Mawaziri hawana instruments, hakuna mawaziri.” Alisema kiongozi huyo wa ACT.

Hata hivyo aliwaasa Wabunge katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kuwa Bunge la 11 lazima liwe tofauti na Mabunge yaliyopita, kwani yalikuwa na kazi ya kupambana na ufisadi kwa sababu Serikali iliyopita ilionekana kutofanya kazi hiyo vizuri.

“…Bunge lilijipa kazi ya ‘kutumbua majipu’ na kuilazimisha Serikali kutekeleza Maazimio ya Bunge. Hivi sasa kazi hiyo ya kutumbua majipu inafanywa na Serikali yenyewe, inafanywa na Rais mwenyewe. Hivyo Bunge lazima litafute wajibu mpya katika kipindi hiki.”

“…Bunge na hasa wabunge wa upinzani lazima sasa kutazama njia mbadala za kuifanya Serikali iwajibike. Kwa mfano, ni dhahiri nafasi ya wazi kabisa ni katika kuanisha mwelekeo wa nchi na kujenga mfumo madhubuti wa uwajibikaji. Ni lazima kubadilika na kubadili aina ya siasa. Tusifanye mambo yanayotarajiwa; kwa mfano kutoka tu bungeni halafu tunarudi tena.”

“…Kama Serikali inaenda kinyume na sheria, katiba na kanuni, kwa nini tusifanye mikutano ya wananchi, bunge la wananchi ambapo tunajadili kwa uwazi mambo yanayotusibu. Tunaweza kutumia vizuri digital technology kuhakikisha ujumbe wetu unafika kwa wananchi bila kujali kama TBC wanaweka live au la. Ni lazima tuwe innovative katika Siasa. Tusifanye siasa za kila siku.” Alieleza Zitto katika hotuba hiyo.

Soma zaidi hotuba zima ya Zitto katika ukurasa wetu wa Thehabari.comm