ALIYAUWA Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe ametaja sababu tano za kujiunga na chama cha ACT-Tanzania huku akijigamba kuwa yeye ni mchapakazi na kwamba sasa mambo yote ni mbele kwa mbele. Akimnukuu Rais wa zamani wa Ghana, Hayati Kwame Nkrumah aliyewahi kusema, ‘forward forever, backward never’, jana Zitto alisema, sasa ni wakati wa kuangalia mbele, hakuna kurudi nyuma tena huku akijisifu kwa umahiri wake katika kazi.
“Mimi ni mchapakazi…siangalii nyuma tena, naangalia mbele. Mapambano yanaanza matokea mtayaona baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu,” alisema Zitto kujiamini.
Zitto ambaye aling’atuka kutoka kwenye nafasi ya Ubunge Ijumaa iliyopita kupitia Chadema na kujiunga na chama ACT siku moja baadae, alisema watu wengi wamekuwa nini kingefuata baada ya ya kuachia nafasi.
“Sasa napenda kuwaarifu kuwa Machi 20, mwaka huu siku ya Jumamosi nilijiunga na chama cha ACT na kukabidhiwa kadi ya uanachama na mwenyekiti ACT, Tawi la Tegeta. Hii ilikuwa moja katika siku muhimu kabisa katika maisha yangu ya kisiasa,” alisema Zitto na kuongeza kuwa amelipa ada ya uanchama hadi mwaka 2025.
Zitto ambaye pia alikuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), alifunguka na kueleza sababu za kuhamia katika chama hicho ambacho kimenzishwa juzi na siyo chama kingine cha siasa, kama ambavyo watu wengi wanajiuliza.
“Nimejiunga na ACT kwa sababu ninaona kwamba huku ndiko kunakaoendana na kile ambacho mimi nimekipigania kwa miaka yote tangu nianze siasa, ambacho nikuweka maslahi ya taifa mbele dhidi ya kitu kingine chochote,” alisema Zitto huku akishangiliwa na baadhi ya wanachama wa chama hicho waliohudhuri mkutano huko.
Alisema sababu nyingine ni kwamba ACT ni chama pekee nchini kinachokubaliana na Itikadi ya Ujamaa na kinaamini katika Falsafa ya Unyerere. Aliongeza kuwa, amejiunga na chama hicho kwa sababu ni chama kinachoamini katika msingi wa uadilifu na kimeweka miiko ya maadili ya uongozi katika kuhakikisha kwamba viongozi wote wa ACT wanakubaliana nayo na wanaisaini.
“Naamini kuwa na miiko na maadili kwa viongozi ni mwanzo wa kuhakikisha kwamba jamii yetu inaishi katika uadilifu na kwamba viongozi wanakuwa na audilifu katika jamii,” alisema.
Aliongeza; “Mtakumbuka kwamba katika miaka yangu yote ya ubunge nimepigania uwajibikaji na uwazi. Hii ni misingi ambayo ninaamini kwamba ni moyo wa utashi na umma,”
Alisema amafurahi kwamba kati ya misingi kumi ya chama chake kipya, uwajibikaji na uwazi ni sehemu muhimu. Uwazi ni sehemu ya jina la chama hicho.
Naye, Msanii wa muziki wa Hip Hop, Seleman Msindi ambaye alikuwa mwanachama wa Chadema, aliunga mkono hoja ya msemaji huyo na kusema kuwa Chadema haikufanya jambo la busara kumfukuza Zitto.
Wanachama wengine wapya ni pamoja na aliyewahi kuwa mgombea wa kura za maoni 2010, Askofu Gerald Mpango, aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Sheria na Haki za Binadamu Kanda ya Magharibi, Jaji Mstaafu Musa Kwikima, aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema mkoa wa Tabora, Kansa Mbarouk.
Aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema Wilaya ya Kaliua, Jorum Mbogo, aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Tabora na Mjumbe wa Kamati Kuu, Meck Mzirai, aliyekuwa Mwenyekiti wa Jimbo la Kahama kwa kiti cha Chadema, Charles Lubala, Diwani wa Halmashauri ya Mabogini, Moshi vijijini kwa kiti cha Chadema, Albert Msando.
Aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Iringa, Dokta Ben Kapwani, aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Katavi, John Mallac, aliyekuwa Kaimu Mwenyekiti wa TLP Mkoa wa Mbeya na Mwenyekiti Wilaya ya Mbarali Mwasimtwa Mwagongo na Katibu wa TLP Wilaya ya Mbarali Seleman Nyumile.
CHANZO:- http://www.mwananchi.co.tz