ALIYEKUWA Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, Zitto Kabwe ameshinda maombi yake dhidi ya chama hicho mahakamani. Katika maombi hayo namba 1 ya mwaka 2014, Zitto ambaye pia ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini, aliiomba Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam kuizua Kamati Kuu (CC) ya Chadema kumjadili au kuchukua uamuzi wowote kuhusu uanachama wake.
Zitto kupitia kwa Wakili Albert Msando alikuwa akiiomba Mahakama itoe zuio hilo la muda hadi kesi yake ya msingi itakaposikilizwa na kutolewa uamuzi. Katika uamuzi wake jana, Mahakama Kuu ilikubaliana na maombi na hoja za Zitto na kutoa zuio kwa Kamati Kuu ya Chadema na au chombo chake chochote cha uamuzi kumjadili na kutoa uamuzi wowote kuhusiana na uanachama wake, hadi kesi yake ya msingi itakaposikilizwa na kuamuliwa.
Awali, Mawakili wa Chadema wakiongozwa na Mwanasheria Mkuu, Tundu Lissu na Mkurugenzi wa Katiba, Sheria na Haki za Binadamu, Peter Kibatala walipinga maombi hayo wakidai kuwa hayajakidhi matakwa ya kupewa zuio la muda. Katika uamuzi wake, Jaji John Utamwa alikubaliana na hoja za Wakili Msando kuwa maombi hayo yametimiza matakwa yote ya kupewa zuio hilo.
Matakwa hayo ni pamoja na kuwapo kwa mgogoro baina ya pande mbili, hasara au madhara yasiyoweza kufidiwa na usawa katika athari kwa pande zote. Jaji Utamwa alikubaliana na hoja za Wakili Msando kuwa iwapo Mahakama haitaingilia kati na kutoa zuio hilo, mtoa maombi ataathirika zaidi kuliko wajibu maombi.
Akijibu hoja ya Wakili Lissu aliyepinga hoja ya mtoa maombi kuathirika pamoja na wananchi wa jimbo lake kwa kukosa uwakilishi bungeni, kuwa hata akipoteza ubunge kwa kuvuliwa uanachama utaitishwa uchaguzi mdogo, Jaji Utamwa alisema uchaguzi mdogo huwa unachukua mchakato mrefu.
Baada ya kurejea vifungu mbalimbali vya sheria, kanuni, amri na uamuzi wa kesi mbalimbali za Mahakama Kuu, Mahakama ya Rufani na za nje, Jaji Utamwa alisema anakubaliana mtoa maombi.
“Kwa hiyo ninatoa zuio la muda kwa Kamati Kuu ya Chadema na au chombo chake chochote cha uamuzi kwamba kisimjadili na kutoa uamuzi wowote dhidi ya mleta maombi kuhusiana na uanachama wake kusubiri kusikilizwa na kuamuriwa kwa kesi yake ya msingi,” alisema Jaji Utamwa.
Kabla ya kufikia uamuzi huo, Jaji Utamwa alitupilia mbali hati ya kiapo kinzani ya Chadema iliyotolewa na Wakili Kibatala baada ya kuwekewa pingamizi na Wakili Msando ambaye alidai kuwa katika hati hiyo, kuna taarifa za kusikia ambazo hakueleza alipozitoa.
Huku akirejea vifungu vya sheria, kanuni, amri na uamuzi wa Mahakama mbalimbali, alisisitiza kuwa ingawa wakili anaweza kuapa kwa niaba ya mteja wake, lakini anapaswa kueleza chanzo cha taarifa anazozitoa katika kiapo hicho.
Baada ya kutupilia mbali kiapo hicho, Jaji Utamwa alisema hata vielelezo vya wajibu maombi vinakufa kifo cha kawaida na kwa hali hiyo, maombi ya mtoa maombi yanabaki bila kupingwa na kwamba hakuna haja pia ya kujadili hoja za upande wa wajibu maombi.
Baada ya Jaji kutoa uamuzi huo, Zitto, aliwafuata mawakili wa Chadema na kupeana nao mikono kisha akaongozwa na walinzi wake kutoka nje ya Ukumbi wa Mahakama akipitia mlango maalumu unaotumiwa na jaji.
Kabla ya hukumu
Zitto aliyekuwa amevalia suti ya kijivu na shati la michirizi myeupe na ya kijivu aliwasili mahakamani hapo saa 7:45 mchana akiongozana na walinzi wake binafsi (mabaunsa), wapambe na wakili wake. Baada ya kufika alikwenda katika chumba maalumu ambako alipumzika hadi saa 9:45 alasiri alipoingia katika ukumbi na kukaa katikati ya wapambe wake huku nyuma yake wakiwapo walinzi wake.
Jaji Utamwa aliingia mahakamani saa 9:56 alasiri na kuanza kusoma uamuzi wake akianzia na pingamizi la Zitto kwenye hati ya kiapo kinzani cha Chadema kisha akamalizia na uamuzi wa maombi ya msingi. Hukumu hiyo ilimalizika kusomwa saa 11:10 jioni.
Baada ya hukumu
Akizungumza baada ya uamuzi huo, Wakili Msando alisema wameupokea kwa furaha uamuzi huo wa mahakama na kwamba hiyo ni hatua mojawapo ya haki akisema anaamini kuwa mteja wake atapata haki anayoitafuta.
Hata hivyo, Lissu na Kibatala kwa nyakati tofauti walisema kuwa ingawa wanakubaliana na uamuzi huo, hajawaridhika. Maombi hayo ya Zitto yaliyotolewa uamuzi jana yanatokana na kesi ya msingi aliyofungua mahakamani hapo Januari 2, mwaka huu, dhidi ya Bodi ya Wadhamini wa Chadema na Katibu Mkuu wa Chadema.
Katika kesi hiyo anaiomba Mahakama izuie chama hicho, wakala wake na vyombo vyake vya uamuzi kumchukulia hatua zozote wala kumjadili kuhusiana na uanachama wake, hadi hapo rufaa anayokusudia kuikata Baraza Kuu la Chadema kupinga kuvuliwa nyadhifa zake itakaposikilizwa.
Kesi hiyo ya msingi imepangwa kutajwa Februari 13, 2014.
Mapambano tena
Wafuasi wa Chadema wanaomuunga mkono Zitto na wale wa uongozi wa juu, jana walipambana tena mahakamani kwa ngumi na mawe kisha kusababisha watu wawili kujeruhiwa. Vurugu hizo zilitokea saa 7.55 mchana muda mfupi baada ya Zitto kuingia mahakamani. Katika vurugu hizo, mmoja wa wafuasi hao ambaye jina lake halikujulikana mara moja, aliumizwa kichwani baada ya kupigwa na jiwe na mwingine alipigwa jiwe tumboni na kupelekwa hospitali.
Kutokana na vurugu hizo, polisi waliyatenganisha makundi hayo katika sehemu tofauti na kukaa katikati ili kuyatenganisha. Wakati Zitto akiwasili mahakama hapo, wafuasi wake walikuwa wakiimba `Zitto Zitto kama Mandela’ hali iliyowalazimu wafanyakazi wa Mahakama kuingilia kati na kuwazuia.
Makundi hayo ya wafuasi wa chama hicho yalifika mapema saa 6:30 mchana mahakamani hapo kusikiliza uamuzi uamuzi wake. Ulinzi katika eneo lote la Mahakama uliimarishwa, makundi ya polisi wa kawaida na wale wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU), waliokuwa na silaha pamoja na mabomu ya machozi walitanda sambamba na askari wa kikosi cha mbwa, magari manane ya polisi na matatu ya maji ya kuwasha.
Kama ilivyokuwa juzi, ni wafuasi wachache walioruhusiwa kuingia ndani ya chumba cha Mahakama.
Baada ya mahakama kutangaza uamuzi wake, wafuasi wa Zitto walishangilia kwa nguvu na kuondoka wakiimba nyimbo za kumsifu kiongozi huyo.
Mtei amwonyesha mlango Zitto
Mwasisi wa Chadema, Edwin Mtei amemtaka Zitto aunde chama chake au atafute kingine cha kujiunga nacho kwa kuwa kwa sasa hana nafasi. Pia ameshauri kuwa kama ana ndoto za kuwania urais ni vizuri akatafute vyama vingine kama CCM au CUF kwa kuwa ndani ya Chadema kwa sasa hahitajiki.
Mtei alisema kuwa kama anataka kubakia na uanachama wa Mahakama wao hawana shida… “Lakini huwezi kuwapeleka viongozi wako kortini na bado ukaendelea kubaki kuwa mwanachama wetu.”
Alimtuhumu kwa kuwagonganisha viongozi mbalimbali ndani ya Chadema na hata kuzua mitafaruku ya hapa na pale huku akisema kwamba uamuzi wa Kamati Kuu ndiyo wa mwisho.
Mwenyekiti wa Chadema Wilaya ya Temeke atekwa nyara, ajeruhiwa
Mwenyekiti wa Chadema, Wilaya ya Temeke, Joseph Yona (32), ametekwa nyara na kujeruhiwa vibaya kwa kipigo kisha kutupwa katika vichaka eneo la Tegeta Ununio, wilayani Kinondoni a watu wasiojulikana.
Yona ambaye alitekwa juzi akiwa katika eneo la Mtoni kwa Aziz Ali, amelazwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili. Yona ambaye pia ni Mjumbe wa Baraza Kuu la Chadema alisema jana kwamba alitekwa yapata saa 5.00 usiku wa kuamkia jana na watu ambao awali, walijitambulisha kuwa ni polisi.
“Tulikuwa tumekaa na vijana wanne wa Tawi la Ukombozi, Chadema la Temeke, ndipo ghafla wakajitokeza watu kama sita hivi wakaja moja kwa moja na kuninyanyua huku wakiniambia twende kituo cha polisi,” alisema.
Alisema baada ya kuingia ndani ya gari ambalo lilikuwa linafanana na yale ya polisi alivuliwa fulana na kufungwa macho na mikono. Alisema baada ya mwendo uliochukua kitambo kidogo, gari hilo lilisimamishwa na watu hao wakamshusha chini na kumpeleka sehemu iliyokuwa na bonde huku wakiendelea kumpiga kabla ya kumtelekeza na kutoweka.
“Njiani nilijaribu kuwasihi wasiniue kwa kuwa nina watoto wadogo wawili ambao wananihitaji, niliwasisitiza watambue na kwamba nao wana watoto wafikirie, wakaniuliza kwa nini naivuruga Chadema kwa tamko nililolitoa hivi karibuni kutokana na mgogoro unaoendelea,” alisema.
Alisema kuwa alijitetea kwa kuwataka wakasome vizuri tamko lake, lakini waliendelea kumpiga na kumtaka aombe msamaha kwa kuishambulia Kamati Kuu ya chama hicho, jambo ambalo hakuwa tayari kulifanya kwa kuwa hakuona kama kuna kosa alilolifanya.
“Walinitupa na kutimua mbio wakiniacha nikiwa na maumivu makali. Nilitulia kwa muda na kujitahidi kuinuka na kupiga hatua kwenda nyumba zilizokuwa jirani kuomba msaada, hapo sikuwa na simu wala nauli,” alisema.
Alisema kuwa alipata msaada wa fulana na kuwasiliana na ndugu zake na polisi ambao baada ya muda walifika na kumpeleka Muhimbili kwa matibabu. Hivi karibuni, Yona alitoa tamko la kupinga hatua ya Zitto kuvuliwa nyadhifa zake na Kamati Kuu ya chama hicho.
Kova aunda jopo la uchunguzi
Kamanda wa Polisi, Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova alisema jana kuwa ameunda jopo la wapelelezi wanane watakaoongozwa na Mkuu wa Upelelezi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Jaffari Mohamed kuchunguza tukio hilo.
Chadema yalaani
Kwa upande wake, Chadema kimeeleza kupokea kwa mshtuko taarifa za tukio la kutekwa, kuteswa na kuumizwa kwa Yona. Katika taarifa yake iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano na Uhusiano, chama hicho kimeliomba Jeshi la Polisi kufanya uchunguzi wa tukio hilo kililoliita kuwa ni la kihuni na mengine ya namna hiyo yenye lengo ya ukatili dhidi ya binadamu, ili ukweli ujulikane na haki itendeke kwa sheria kuchukua mkondo wake.
Pia kimewataka wanachama na Watanzania kwa ujumla kutulia, hasa pale watu wenye hila na malengo yao wanapoanza kukihusisha na tukio hilo.
CHANZO: Mwananchi