Na Joachim Mushi
MBUNGE wa Chadema na Naibu Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Zitto Kabwe amesema hawezi kufanya maamuzi magumu ya kutoka ndani ya chama hicho kwa kile kilichotokea ndani ya chama hicho. Amesema yeye atakuwa wa mwisho kutoka Chadema na si vinginevyo. Zitto ameyatoa hayo leo katika mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam alipokuwa anazungumzia maamuzi ya Kamati Kuu ya Chadema ya kumvua nafasi zake zote za uongozi yeye pamoja na Mjumbe wa Kamati Kuu ya chama hicho Dk. Kitilla Mkumbo na aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema Mkoa Arusha Samson Mwigamba. Zitto amekana kuhusika wala kuujua waraka wa siri ambao ndiyo uliosababisha kumvua madaraka baada ya uamuzi wa Kamati Kuu ya chama kuunasa waraka huo.
“Mimi nimeusikia ule waraka kwa mara ya kwanza kwenye Kamati Kuu na nilisikitika sana kwanini hukunifikia haraka kwani ningeanza kutekeleza mara moja.” alisema Zitto akizungumza.
Huenda leo watu walitegemea nitafanya maamuzi magumu ya kuondoka kwenye chama; “Mimi bado ni mwanachama wa Chadema na nitakuwa wa mwisho kutoka kwenye chama hiki kwa hiyari yangu, nitafanya taratibu zote za chama kuhitimisha jambo hili mimi sitoki kwenye chama hiki labda wanitoe wao,” alisema Zitto.
Zitto alisema anaumia sana anapotuhumiwa kwa kuwa yeye ni binadamu. “…ninapotuhumiwa naumia ninapoambiwa naujumu chama hiki naumia kwa kuwa nakipenda chama na nimekitumikia muda mrefu. Aidha aliwataka viongozi wa Chadema kuacha siasa za uzushi ili kujenga chama himara na kuwakomboa Watanzania.
“…Sisemi kama mimi sina makosa ni binadamu nimefanya mambo mengi kwa chama changu, lakini kinachoendelea kwa sasa ndani ya chama chetu ni mapambano ya kukuza demokrasia na ni mapambano ya wanaotaka mabadiliko na wasiopenda mabadiliko ndani ya chama…mapambano ya wawajibikaji na wasiopenda kuwajibika ni mapambano ya wanaopenda demokrasia na wanaokwaza demokrasia.” alisema Zitto huku akionesha kusikitishwa.
Kwa upande wake Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Dk. Kitilla Mkumbo aliyevuliwa nafasi hiyo hivi karibuni amekiri kuandaa waraka wa siri ambao ulikuwa na malengo ya kufaya mabadiliko ndani ya chama hicho. Dk. Kitilla amesema waraka wa siri ulisambazwa na baadhi ya viongozi wa chama chao ni kweli waliuandaa wao pamoja na mwanasiasa mwingine ambaye hakumtaja na amesema endapo mwenyewe atapenda atajitaja.
Hata hivyo tayari Mtandao wa dev.kisakuzi.com umelipata jina la mwanasiasa huyo ambaye alishirikiana na Dk. Mkumbo kuandaa waraka huo. Dk. Mkumbo alisema suala la kuwa na mikakati ya mabadiliko kwenye chama ni suala la kawaida lakini huandaliwa kwa siri pasipo kukigawa chama.
“…Suala la kuwa na mikakati ya mageuzi kwenye chama kwa siri ni kitu cha kawaida na kinafanyika popote ilimradi kisiasiri taasisi…tutajidanganya tukisema kwamba viongozi ndani ya Chadema hawana mikakati yao ya kiushindani halali wa kidemokrasia ndani ya chama. Hii ipo kila sehemu ya demokrasia.
“…Mkakati huu ulikuwa na malengo mazuri ya kuleta mabadiliko ya kidemokrasia tofauti na unavyofikiriwa na viongozi wa chadema.” alisema Naye Mwanasheria wa Zitto amesema Kamati Kuu ya Chadema imefanya maamuzi kinyume na katiba ya Chadema ya kuwavua nafasi za uongozi wanachama hao bila kufuata taratibu na sheria. “…Tunamtaka Mwanasheria wa Chadema aseme ni lini waliovuliwa uongozi walipewa onyo au kuandikiwa mashtaka yao kwa barua na kupewa muda wa kujitetea kabla ya kuwahukumu.
“…Tunataka mwanasheria aseme tunataka aseme ni lini ameona Zitto amehusika kwenye uandaaji wa waraka huo. Tunataka aseme kama kuna mashtaka yoyote ambayo yameshatolewa kwa maandishi na chama juu ya tuhuma hizo zaidi ya kusikia kwenye mtandao na vyombo vya habari, lakini endapo watapewa maandishi ya mashtaka watajitetea. Utaratibu haujafuatwa,” alisema.