Zitto aomba achunguzwe na vyombo vya dola kuhusu rushwa

Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Kabwe Zitto (CHADEMA)

*Ni kuthibitisha tuhuma za rushwa dhidi yake

MBUNGE wa Kigoma Kaskazini, Kabwe Zitto (CHADEMA) amevitaka vyombo vya dola na mamlaka nyingine stahili zimchunguze dhidi ya tuhuma zinazotolewa dhidi yake kwamba amechukua rushwa pamoja na baadhi ya wabunge wengine.

Kiongozi huyo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC), ameahidi kujiuzulu nafasi ya uongozi katika kamati hiyo endapo itadhihirika kuwa amepokea hongo kutoka eneo lolote.

Zitto ametoa kauli hiyo leo mjini Dodoma alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kutoa ufafanuzi juu ya tuhuma anuai zinazotolewa dhidi yake pamoja na kuelezea mlolongo mzima uliofanywa na kamati yake.

“Nalazimika kukutana nanyi kutoa maelezo juu ya tuhuma zenye shinikizo la kisiasa zinazoelekezwa kwangu binafsi kwamba hata mimi nimeshiriki katika vitendo vya rushwa, kwa nafasi yangu kama Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Mashirika ya Umma. Taarifa hizo, kama kawaida ya uzushi mwingine wowote zimesambazwa kimkakati na kwa kasi kubwa kiasi cha kuukanganya umma.”

“Nafahamu nabeba dhamana kubwa ya uongozi, taswira yangu ya uongozi daima imeakisi njozi na matumaini ya wananchi wa Kigoma Kaskazini, wananchi wanyonge na vijana kote nchini bila kujali itikadi zao za kisiasa, jinsia zao, makabila yao na rika zao.”

“Hivyo, nawajibika kupitia kwenu kuwatoa hofu juu ya hisia potofu zinazopandikizwa kwao na wale wasiopenda kuona baadhi yetu tukiwaunganisha na kuwasemea watanzania wasio na sauti, dhidi ya vitendo vya hujuma na vyenye dhamira ovu kwa taifa.”

Alisema kumekuwa na mkakati wa kumuunganisha na baadhi ya Waheshimiwa Wabunge wanaotuhumiwa kwa kupokea Rushwa unatekelezwa kwa njia mbalimbali, ikiwemo kauli za watendaji wa Serikali ambao wamekuwa wakieneza na hususan kutoa taswira kwamba baadhi ya kauli za mbunge huyo zinatokana na ushawishi wa rushwa.

“Kuna taarifa ambazo zimeandikwa tena katika kurasa za mbele za baadhi ya vyombo vya habari zikidai” Zitto kitanzini” ama ‘Zitto sawa na popo nundu” zikiashiria kwamba na mimi ni mla rushwa; na Waandishi wa habari na jamii kwa ujumla wamefikia kuaminishwa habari hizi kiasi cha wengine kuuliza kwa nini Mhe. Zitto Kabwe hakutajwa katika orodha iliyotolewa na Mnadhimu Mkuu wa Kambi ya Upinzani.”

Aidha alisema mara baada ya bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Usambazaji wa Umeme Tanzania (TANESCO) chini ya Uenyekiti wake Meja Jenerali mstaafu, Robert Mboma kutangaza kumsimamisha kazi Mkurugenzi Mkuu wa Shirika hilo, William Mhando kupisha uchunguzi wa baadhi ya vitendo/mwenendo wake.

Alisema kamati yao ya POAC ilimuandikia Spika kumuomba aridhie ili Kamati iweze kuwaita Bodi ya TANESCO, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Mahesabu ya Serikali (CAG) na pia Mamlaka ya Udhibiti wa Manunuzi ya Umma (PPRA) kujiridhisha na tuhuma zote zinazotajwa zinafanyiwa uchunguzi wa kina na hatua kuchukuliwa.

Kamati ya POAC chini ya uongozi wake ilimuomba Spika kuwaita wahusika hao kwa kuwa kulikuwa na tetesi kwamba kusimamishwa kazi kwa Mkurugenzi huyo siku chache kabla ya Bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini kulikuwa na lengo la kufunika ’madudu’ makubwa zaidi kwa kulichagiza Bunge na tukio hilo dogo, mkakati ambao alidai ulifanikiwa kiasi kikubwa.

“Kitendo hiki cha halali na kwa mujibu wa Kanuni kilichofanywa na Kamati yangu kimetafsiriwa kwa makusudi na baadhi ya watu kwamba ni ishara ya kuwa sisi au zaidi kwamba mimi nina maslahi binafsi na TANESCO na hususan Mkurugenzi wake Injinia Mhando, ndio maana tumetaka maelezo ya Bodi. Ukweli kwamba Kamati ya POAC tumewaita pia Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Mahesabu (CAG) na Mamlaka ya Udhibiti wa Manunuzi ya Umma (PPRA) kwa jambo hilo hilo umefichwa kwa makusudi.”

“Baada ya tukio hilo, nikiwa hapa Dodoma, mwandishi wa habari wa gazeti moja alinifuata akiniambia kuwa wamekutana na Mhe. Waziri Mhongo na Katibu Mkuu wake, Nd. Eliachim Maswi hapa hapa Bungeni na wamewaambia kuwa mimi nimepewa rushwa. Hakutaja nimepewa rushwa na nani, kiasi gani na wala kwa lengo gani,” alisema Zitto.

“…Binafsi sijawahi kuwa na mawasiliano ya aina yeyote na uongozi wa TANESCO kushawishiwa juu ya hatua ambazo POAC ndio imezichukua za kutaka kujiridhisha juu ya utaratibu uliotumika. Ieleweke wazi kabisa kuwa, hakuna wakati wowote, popote ambapo mimi binafsi au Kamati yetu imekataa Mkurugenzi Mkuu wa TANESCO kuchunguzwa kwa tuhuma zozote. Ambacho tumesisitiza wakati wote ni ufuatwaji wa taratibu, kanuni na sheria, hili nitalisimamia iwe masika au kiangazi,” alisema.

“Natumia fursa hii pia kuomba vyombo vya Dola vichunguze tuhuma hizo kwa nafasi yake ili kuweza kupata ukweli. Ninaahidi kushiriki kikamilifu iwapo nitatakiwa katika uchunguzi wowote utakaofanywa na niko tayari kuwajibika iwapo nitakutwa na hatia yeyote. Napenda niwatoe hofu wananchi wa jimbo la Kigoma Kaskazini walionituma kuja kuwawakilisha hapa Bungeni na Watanzania wote kwa ujumla kwamba,”

“Mimi Zitto Zuberi Kabwe sina bei, sijawahi kuwa nayo na sitarajii kuwa nayo huko mbeleni. Daima nimesimamia kidete maadili ya uongozi bora katika maisha yangu yote ya siasa, na nawaahidi sitarudi nyuma katika mapambano dhidi ya rushwa katika nchi hii pamoja na mikakati ya aina hii ya kunidhoofisha na kunivunja moyo…” alisema Zitto katika taarifa yake.