Joto la kisiasa katika Jimbo la Kigoma Kusini, linazidi kupanda, baada ya baadhi ya viongozi wa Chama cha NCCR-Mageuzi kutoka makao makuu kuingia jimboni humo wakieleza hatua zilizochukuliwa na chama hicho dhidi ya Mbunge wa jimbo hilo, David Kafulila .
Viongozi hao ambao wamepata wakati mgumu wakati wakifuatilia ziara ya Kafulila kwa zaidi ya wiki moja tangu alipoanza ziara ya kuzungumza na wananchi kuwaeleza uamuzi wa Halmashauri Kuu (NEC) kumvua uanachama.
Viongozi hao wamenusurika kupigwa na wafuasi wa Kafulila kutokana na kutokubaliana na maamuzi hayo.
Kwa zaidi ya wiki moja, Mwenyekiti wa Makamishna wa NCCR-Mageuzi Taifa, Peterson Mshenyela, ambaye pia ni Kamishna wa Mkoa wa Kagera akiwa na afisa wa chama hicho, Hemed Msabaha, wamekuwa wakitembelea matawi ya chama hicho katika Tarafa ya Nguruka na kugawa nyaraka za chama hicho na kueleza kuwa Kafulila ni mbunge wa Mahakama.
Nyaraka wanazozisambaza ambazo gazeti hili linazo ni barua inayodaiwa kuandikwa na Kafulila kuomba radhi baada ya NEC kumvua uanachama na hati ya maamuzi ya Mahakama Kuu inayokielekeza chama hicho kutochukua hatua zaidi dhidi ya Kafulila hadi kesi ya msingi ya kupinga kuvuliwa uanachama iliyofunguliwa na Kafulila itakaposikilizwa.
Mshenyela alipoulizwa uwepo wao na kazi wanayofanya katika jimbo hilo, alisema wanatembelea matawi ya chama hicho kwa lengo la kuimarisha chama.
Hata hivyo, viongozi hao juzi, walipata wakati mgumu walipofika nyumbani kwa Diwani wa Kata ya Nguruka, Abdalah Masanga, baada ya kundi la wafuasi wa chama hicho kuwazingira na kutaka kuwapiga, hali iliyowalazimu kukimbilia kituo cha polisi Nguruka.
Kufuatia tukio hilo, viongozi hao wa NCCR-Mageuzi, walimfungulia kesi Katibu Kata wa chama hicho katika Kata ya Itebula, Thobias Kichwa, kwa madai ya kutishiwa kuuawa na kuchukuliwa bendera ya chama hicho kinyume cha taratibu.
Akizungumza kwa njia ya simu toka Nguruka, Kichwa, alisema ameshitakiwa kituo cha polisi Nguruka na Msabaha kwa kosa la kutishia kumuua yeye na Mshenyela na kwamba wao hawakubaliani na mambo na propaganda zinazoenezwa na viongozi hao kutoka makao makuu.
Akizungumzia hali hiyo, Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi wa kijiji cha Nyangabo katika Kata ya Nguruka, Simon Katenza, alisema wanawaomba watu hao waondoke katika jimbo hilo na kuacha kuwalaghai wananchi na kuwachonganisha na mbunge wao.
Wakati hali hiyo ikitokea, Kafulila, anaendelea na ziara katika jimbo lake pamoja na mambo mengine kuwaeleza wananchi mikakati na utatuzi wa kero mbalimbali zinazowakabili.
Juzi katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Kata ya Nguruka, viongozi wa serikali za vijiji na madiwani walitoa tamko la kujiondoa kwenye chama hicho ikiwa mbunge wao atavuliwa uanachama na kupoteza ubunge.
CHANZO: NIPASHE