Na Mwandishi Wetu, Rombo
WAKULIMA wa zao la kahawa wilayani Rombo wametahadharishwa kuwa upo uwezekano wa zao hilo kukosa soko kutokana na wakulima wengi eneo hilo kwa sasa kutofuata kanuni za kilimo cha zao hilo hususani kipindi cha mavuno. Hayo yameelezwa na Mwenyekiti wa Chama cha Msingi cha Ushrika wa Kilimo na Mazao Mashima (AMCOS), Atanasi Silayo wakati alipokua akifungua mkutano mkuu wa mwaka wa chama hicho.
Silayo alisema kuwa wakulima wengi wilayani humo hawafuati kanuni bora za kilimo cha kahawa na hivyo kusababisha ubora wa zao hilo kupungua na kushuka bei kila wanapozipeleka mnadani wakati wa kuvuna. Silayo aliwataka wakulima kufuata taratibu za kilimo bora kuanzia shambani hususani wakati wa kuvuna ili kuongeza ubora wa kahawa suala ambalo litaongeza pia bei ya kahawa na kuinua uchumi wa chama na kipato kwa wakulima kwa ujumla.
Kwa upande wao wakulima wakizungumza wakati wa mkutano huo wamesema ni vyema Serikali pamoja na halmashauri kuwasaidia ili kupata wataalamu wa zao hilo waweze kuzalisha kahawa bora na nyingi badala ya kuacha wakulima kujitegemea wenyewe.
Walisema halmashauri inajipatia mapato mengi yanayotokana na ushuru wa mauzo ya kahawa hivyo ina kila sababu ya kuchangia uboreshaji wa zao hilo, jambo ambalo pia litaboresha kipato cha halmashauri.
Naye Mratibu wa zao la Kahawa Halmashauri ya Wilaya ya Rombo, Mama Shine alisema Halmashauri ya Rombo inatambua umuhimu wa zao la Kahawa hivyo ina lengo la kuboresha zao hilo pamoja na kuongeza wingi na ubora wa zao.
Hata hivyo, kwa upande wake Ofisa Ushirika wa Halmshauri ya Wilaya ya Rombo, John Kabata aliwataka wajumbe wa mkutano huo kukuza mtaji wa ndani wa chama chao kwa kununua hisa ili vyama hivyo viweze kujiendesha vyenyewe badala ya kutegemea mikopo kutoka katika mabanki.