Na Mwandishi wa EANA
RAIS wa Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein amesisitiza umuhimu kwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kuzingatia utawala bora, kwani ni nguzo muhimu katika kuleta maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Dk. Shein alisema hayo jana alipokuwa akifungua mkutano wa mawaziri wanaoshughulikia mambo ya nje, utawala bora na katiba mjini Zanzibar, huku akipongeza uamuzi wa kuanzisha mchakato wa viwango katika utawala bora.
Mkutano huo wa siku tatu umelenga kupita rasimu ya itifaki ya utawala bora kwa nchi wanachama wa EAC. “Wazo la kutengenezwa kwa fomula ya rasimu ya itifaki ya utawala bora ni lazima liwe ni la wadau wenyewe wa Afrika Mashariki,” alisema katika hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Idd.
Hata hivyo kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa waandishi wa habari na sekretarieti ya Afrika Mashariki, Dk. Shein alisema ni vyema rasimu hiyo ya itifaki ya utawala bora ikaoanisha miongozo ya utawala bora ya nchi wanachama wa EAC.
Naye Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri wa EAC na Waziri wa Burundi anayeshughulikia masuala ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, Hafsa Mossi, alisema utawala bora na nguzo zake ni kama kiungo kinacholainisha mchakato wa kuelekea kwenye shirikisho la kisiasa.
“Kuunganika kunahitaji zaidi dhamira ya kisiasa na kuwajibika. Na ni mchakato nyeti kwa sababu unagusa utawala wa kisiasa,” alisema Waziri huyo.
Mkutano huo ulijumuisha wabunge wa Bunge la Afrika Mashariki, makatibu wakuu, wenyeviti wa tume za uchaguzi, wataalamu wa sheria, makamishina wa haki za binadamu, watu wa usalama, mamlaka za kukabiliana na rushwa na vyama vya kiraia.
Mossi alizitaka nchi wanachama kufanya uamuzi hata kama ni mgumu kiasi gani ili kulinda manufaa ya mafanikio ya ushirikiano.
Naibu Katibu Mkuu wa EAC anayeshughulikia Shirikisho la Kisiasa, Beatrice Kiraso, akizungumza katika ufunguzi pia alisema kwamba utawala bora ni muhimu na maamuzi ya mawaziri wa Afrika Mashariki kuandaa itifaki ya Afrika Mashariki ya utawala bora ni hatua kubwa mbele kufikia ushirikiano wa kikanda.
“Kuwekwa kwa viwango vya utawala bora kunasaidia kuanzisha msingi imara wa ushirikiano wa kiuchumi na kisiasa na mwishowe shikrikisho la kisiasa,” alisisitiza Kiraso.
Alisema kwamba ushirikiano wa kisiasa kwa upana wake utasaidia ushirikiano wa kiuchumi. “Ushirikiano wa kiuchuni hauwezi kuondoka ndani ya ushirikiano wa kisiasa kwa hiyo utawala bora ni muhimu katika kusaidia kufikia ushirikiano wa kisiasa wa Afrika Mashariki,’’ alisema Kiraso huku akisisitiza kuwa itifaki hiyo itasaidia katika kuhakikisha kunakuwapo na uwajibikaji na usalama wa ndani.