Zanzibar kuhimarisha sekta ya uvuvi

”] ”]

Na Rajab Mkasaba, Ikulu-Zanzibar

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein amesema kuwa Zanzibar ipo katika mipango kabambe ya kuimarisha sekta ya uvuvi ikiwa ni pamoja na kuhakikisha uvuvi wa bahari kuu unaimarika zaidi.

Kauli hiyo imetolewa leo alipokuwa akizungumza na Balozi wa Jamhuri ya Iran nchini Tanzania, Mohsen Movahhed Ghomi, Ikulu mjini Zanzibar. Alisema Serikali ya Mapinduzi Zanzibar itaendelea kuwapa taaluma wavuvi hasa wavuvi wadogo wadogo ili waendeleze uvuvi na uwe wenye tija na mafanikio katika maisha yao pamoja na kuwa njia moja wapo ya kupambana na umasikini.

Katika maelezo yake, Dk. Shein alisema kuwa kutokana na Zanzibar kuzungukwa na Bahari ni njia moja wapo ya kuwa na rasilimali hiyo kwa ajili ya kuimarisha sekta ya uvuvi hapa nchini ambapo hivi sasa nguvu zaidi zinaelekezwa katika uvuvi wa bahari kuu.

Dk. Shein alimueleza Balozi huyo kuwa Zanzibar inawakaribisha waekezaji wa Jamuhuri ya Irani kuja kuekeza Zanzibar katika sekta mbali mbali ikiwemo sekta ya uvuvi na kusisitiza kuwa lengo ni kuchukua hatua hiyo kwa vitendo kwani soko kubwa lipo la bidhaa hiyo.

Alieleza kuwa Zanzibar itaendeleza uhusiano na ushirikiano wake na Irani huku ikizingatia kuwa uhusiano huoni wa kihistoria ambao hasa ulianzia katika sekta ya biashara kati ya nchi mbili hizo wakati huo.

Dk. Shein alimueleza Balozi huyo kwa Zanzibar imeweka Sera na taratibu nzuri za uwekezaji ili kuweza kuwavutia wawekezaji kuja kuekeza Zanzibar katika sekta mbali mbali za maendeleo huku akisisitiza kuwa Zanzibar ni sehemu yenye amani na utulivu.

Alimueleza kuwa serikali iko tayari kutuma ujumbe wake nchini humo ukiwa na lengo la kukaa pamoja na wawekezaji na wafanyabiashara wa nchi hiyo ili kuweza kukaa pamoja na kupanga mipango na mikakati ya kushirikiana kwa pamoja katika sekta hizo kati ya Zanzibar na nchi hiyo.

Aidha, Dk. Shein alitoa salamu za shukurani kwa Kiongozi Mkuu wa Serikali ya Irani kwa kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika kuimarisha sekta ya kilimo kwa kusaidia pembejeo za kilimo yakiwemo matrekta madogo.

Pia, Dk. Shein alimueleza Balozi huyo kuwa kutokana na Iran kuwa na Taasisi ya Teknolojia itakuwa ni jambo la busara iwapo kutakuwa na mashirikiano mazuri kati ya Taasisi hiyo na Chuo cha Utafiti wa Kilimo Kizimbani hasa katika mambo ya utafiti.

Sambamba na hayo, Dk. Shein aliipongeza nchi hiyo kwa azma yake ya kuiunga mkono Zanzibar katika kuimarisha sekta ya afya na kumueleza juhudi zilizofikiwa hapa nchini katika kuhakikisha wananchi hawatembei zaidi ya kilomita tano kufuata huduma za afya.

Naye Balozi wa Jamhuri ya Irani, Ghomi, alimueleza Rais Dk. Shein kuwa nchi yake inathamini sana uhusiano na ushirikiano uliopo na kumuahidi kuwa hatua za makusudi zitaendelea kuchukuliwa ili kuhakikisha malengo yaliokusudiwa yanafanyiwa kazi kwa vitendo. Alieleza kuwa Iran itaendelea kuziunga mkono juhudi za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika kuimarisha sekta za maendeleo.

Mapema Rais Dk. Shein, alifanya mazungumzo na Balozi wa Saudi Arabia nchini Tanzania, Hani Abdulla Mohammed Mu’minah ambapo katika mazungumzo yao viongozi hao waligusia mambo mbali mbali ya kuimarisha uhusiano na ushirikiano ikiwa ni pamoja na kuendeleza sekta za maendeleo ikiwemo elimu, uwekezaji na nyengineyo.

Katika maelezo yake Balozi huyo wa Saudia alimueleza Dk. Shein kuwa nchi yake itaendeleza uhusiano na ushirikiano kati yake na Zanzibar huku akisisitiza kuwa bado itaendelea kuiunga mkono Zanzibar katika sekta za maendeleo.

Kwa upande wake Dk. Shein alimueleza Balozi huyo kuwa Zanzibar inajivunia uhusiano na Saudia Arabia hali ambayo imepelekea watu wake wakiwemo baadhi ya viongozi wakubwa wa dini hapa nchini kupata mafunzo nchini humo.

Aidha, Dk. Shein alisema kuwa ipo haja ya kuimarisha uhusiano na ushirikiano sanjari na kubadilishana uzoefu wa kimafunzo na kiutaalamu kati ya vyuo vikuu vya Saudi Arabia na Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA).

Alisema kuwa wananchi wengi wa Zanzibar wamekuwa na uhusiano mzuri na Saudi Arabia hasa katika masuala ya kidini. Dk. Shein alimueleza Balozi huyo kuwa Zanzibar itaendeleza uhusiano na ushirikiano wake na Saudia.