Na Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, ameeleza kuwa Zanzibar imeweka milango wazi kwa wawekezaji na wafanyabiashara wa Misri kuja kuekeza na kufanya biashara zao hapa nchini.
Dk. Shein aliyasema hayo leo wakati alipokuwa na mazungumzo na Balozi wa Misri nchini Tanzania, Hossam Eidin Moharam, aliyefika Ikulu mjini Zanzibar kwa ajili ya kujitambulisha kwa Rais.
Katika maelezo yake, Dk. Shein alisema kuwa Zanzibar imeweka milango wazi kwa wafanyabiashara na wawekezaji wa misri kuja Zanzibar kwani hatua hiyo itasaidia kufikia lengo la kukuza uchumi na kuimarisha maendeleo kwa pande zote mbili. Dk. Shein alisema kuwa Zanzibar ina uhusiano na mashirikino ya kihistoroa kati yake na Misri hatua ambayo itasaidia kwa kiasi kikubwa kufikia lengo hilo.
Alisema kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kupitia Mamlaka ya Uwekezaji Vitega Uchumi (ZIPA), iko tayari kutoa ujumbe maalum kwenda kuitangaza Zanzibar pamoja na mazingira yake juu ya sekta ya uwezekezaji na sekta nyenginezo muhimu huko Misri.
Aidha,alieleza kuwa ipo haja ya kukutana wafanyabiashara na wawekezaji wa Zanzibar na Misri kwa lengo la kuzungumza juu ya mashirikiano juu ya sekta ya biashara, uwekezaji na hata sekta ya utalii, hatua ambayo itaimarisha maendeleo na uhusiano zaidi.
Dk. Shein pia, alimueleza Balozi Moharam kuwa ipo haja kwa Shirika la ndege la nchi hiyo ‘Egypt Air Line’ kufanya safari zake hapa Zanzibar kwani hatua hiyo nayo itachangia kuimarisha sekta ya Utalii kwa pande zote mbili.
Alieleza kuwa iwapo kutakuwa na usafiri wa uhakika itakuwa ni jambo la busara kwa kuimarisha sekta ya utalii kwa kuiunganisha miji mitatu mikubwa ikiwemo Cairo, Alexandria na Zanzibar Kiutalii. Dk. Shein alisema kuwa Zanzibar na Misri zimekuwa na uhusiano wa muda mrefu katika kushirikiana juu ya uimarishaji wa sekta za maendeleo zikiwemo Elimu, afya, kilimo na michezo.
Akielezea katika sekta ya elimu, Dk. Shein alisema kuwa Wazanzibari wengi wamepata elimu zao kupitia vyuo mvali mvali vya Misri kikiwemo Chuo Kikuu cha Al-Azhar pamoja na kunufaika na nafasi mbali mbali za masomo ziliokuwa zikitolewa na nchi hiyo yakiwemo mafunzo ya habari na utangazaji.
Pia, Dk. Shein kwa upande wa sekta ya afya, alisema kuwa Misri ilishawahi kuleta madaktari hapa nchini ambao walislishirikiana vyema na madaktari wazalendo katika kutoa huduma za afya hapa Zanzibar.
Akizungumzia kwa upande wa sekta ya kilimo, Dk. Shein alisema kuwa Misri imekuwa na mchango mkubwa katika kuimarisha sekta ya kilimo hapa Zanzibar ambapo imeweza kuchukua juhudi za kuleta wataalamu wa kuja kutoa elimu ya kilimo huko katika shamba la kilimo Bambi.
Alieleza kuwa katika shamba hilo wataalamu wa Misri wamekuwa wakitoa ujuzi mkubwa katika kuimarisha kilimo hasa kilimo cha mbogamboga kwa kutumia utaalamu wa kisasa. Kwa upande wa michezo na utamaduni, Dk. Shein alisema kuwa Misri ni nchi ambayo inaiunga mkono Zanzibar katika kuimarisha sekta ya michezo ambapo nchi hiyo imeweza kuleta waalimu wa kufundisha mpira wa miguu akiwemo kocha wa timu ya Taifa ya Vijana ya Zanzibar.
Nae Balozi wa Misri, Mhe.Moharam alimueleza Dk. Shein kuwa Misri inathamini uhusiano na ushirikiano uliopo wa muda mrefu na kusisitiza kuwa suala zima kuimarisha mashirikiano katika sekta za uwekezaji na biashara nchi yake italipa kipaumbele cha pekee.
Alieleza kuwa uhusiano na mashirikiano sanjari na utamaduni uliopo kati ya Zanzibar na Misri vinaenda sambamba hali ambayo itakuwa ni kivutio kimoja wapo kwa wawekezaji na wafanyabiashara wan chi hiyo.
Balozi huyo alimueleza Dk. Shein kuwa Misri itaendeleza na kuimarisha uhusiano wa pamoja katika kuendeleza sekta za maendeleo ikiwemo kilimo, elimu, michezo na utamaduni pamoja na secta nyenginezo.
Balozi huyo alieleza kuwa kwa kupitia ubalozi mdogo uliopo hapa Zanzibar nchi hiyo itaendelea kuiunga mkono Zanzibar katika kuimarisha sekta za maendeleo na kutoa pongezi kwa mafanikio makubwa yaliofikiwa Zanzibar kiuchumi, kimaendeleo na kisiasa chini ya uongozi wa Dk. Ali Mohamed Shein.