*Sudan, Rwanda wakata tiketi Nusu Fainali
Na Mwandishi Wetu
WAKATI timu za taifa za Sudan na Rwanda zikikata tiketi za kuingia Nusu Fainali ya Mashindano ya Kombe la Tusker Chalenji jana Timu ya taifa ya Zanzibar imeungana na Burundi na kuyaanga mashindano hayo baada ya kukubali kichapo katika michezo miwili ya jana.
Mchezo wa kwanza timu ya Sudan ilifanikiwa kuingia katika hatua hiyo baada ya kuifumua timu ya taifa ya Burundi kwa mabao 2-0. Goli la kwanza la Sudan lilifungwa na mchezaji Amir Rabei Abdelnabi dakika ya 40 ya mchezo, huku Mohamed Musa wa Sudan akihitimisha tena kipigo cha Burundi katika dakika 60 ya mchezo. Kwa matokeo hayo Rwanda sasa inasubiri kuivaa na Sudan katika mchezo wa nusu fainali ambao utafanyika Desemba 8 kwenye Uwanja wa Taifa.
Mchezo wa pili ambao Zanzibar ilikubali kufungwa mabao 2-1 na timu ya Taifa ya Rwanda ulikuwa na ushindani mkali. Goli la ushindi la Rwanda lilifungwa dakika ya 86 mchezo na mchezaji Kagere Meddie aliipatia Amavubi bao baada
ya safu ya ulinzi wa kati ya Wazenji kuzembea.
Mpaka mapumziko Amavubi walikuwa wakiongoza kwa goli 1-0 lililofungwa dakika ya 38 na mchezaji Mugiraneza Baptist akimalizia mpira wa kona iliyochongwa na Haruna Niyonzima. Katika kipindi cha pili Zanzibar itajutia makosa yake kwa kupata nafasi kadhaa na kushindwa kuzitumia.
Zanzibar imepata kona zaidi ya nne pamoja na kupiga mipira ya adhabu zaidi ya mara tatu lakini waliambulia kuitoa nje ya goli, huku wenzao wakiwa wamepata nafasi moja ambayo wakaitumia vizuri na kupata goli.
Heroes ambao waalionekana wakicheza pasi nyingi nyuma pamoja na kumiliki mpira muda mrefu, wachezaji wa timu hiyo walionekana kuridhika
licha ya wao kuwa nyuma kwa magoli. Dakika ya 25 nusura zanzibar ipate goli
kupiti kwa Ali Badru Ali aliyepiga mpira fyongo na kudakwa na kipa akiwa sentimita chache na goli.
Dakika ya 46 ya mchezo Abdulrahim Mohamed aliyeingia katika kipindi hicho cha pili kuchukua nafasi ya Suleiman Kassim, aliipatia Zanzibar bao la kusawazisha hivyo matokeo kuwa 1-1.
Katika mchezo huo Zanzibar iliwakilishwa na Mwadin Ali Mwadin, Nadir Haruob, Juma Othuman/ Amir Hamad Omar, Waziri Salum, Abdilhalim Humud, Suleiman Kassim/Abdulrahim Mohamed, Aggrey Morris, Abdulhalim Gulam/ Ali Kani Mmkanga, Ali Badru Ali, Khamis Mcha Khamis na Ismail Amour.