Zambia na Ivory Coast zatinga nusu fainali

African Cup of Nations 2012

ZAMBIA sasa itacheza na Ghana au Tunisia katika nusu fainali. Zambia ilikuwa timu ya kwanza kujitengea nafasi katika nusu fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika katika mechi ya Jumamosi, baada ya pambano la kwanza la robo fainali kati yake na Sudan, na ilipoondoka na ushindi wa mabao 3-0 katika mechi iliyochezewa uwanja wa Bata.

Stoppila Sunzu aliandikisha bao la kwanza alipofunga kwa kichwa. Mchezo ulianza kuwa mzuri kwa upande wa ghana, hasa baada ya Saif Eldin alipoamriwa na mwamuzi kuondoka uwanjani, alipomchezea vibaya Rainford Kalaba katika lango.

Nahodha Chris Katongo aliweza kufunga bao, licha ya kwamba alifanikiwa baada ya jaribio lake la pili, huku James Chamanga akiandikisha bao la tatu na la kumalizia kazi. Timu ya Chipolopolo sasa itasalia Bata kucheza nusu fainali, ikimsubiri mshindi atakayepatikana katika mechi ya Jumapili, kati ya Ghana na Tunisia.

Hii ni mara ya kwanza kwa Chipolopolo kuwa miongoni mwa timu nne zinazosalia kwa nusu fainali, tangu mwaka 1996. Mechi hiyo ya kwanza ya robo fainali ilianza kwa uwanja mzima kunyamaza kwa dakika moja, ili kuwakumbuka mashabiki 74 waliokufa uwanjani Port Said, Misri, siku ya Jumatano.

Bila shaka ni fahari kubwa kwa kocha wa Zambia, Herve Renard kutoka Ufaransa, kuona kwamba amefanikiwa kuijenga vyema timu ya taifa ambayo iliwapoteza wachezaji kupitia kifo katika ajali ya mwaka 1993 katika pwani ya Gabon.

Ilikuwa ndio ajali mbaya zaidi ya ndege kuwahi kuikumba timu hiyo ya taifa, wakati ilipokuwa ikikisafirisha kikosi cha Zambia kuelekea Senegal kwa mechi ya kufuzu, ilipoanguka, na ikawa ni motisha kwa timu hiyo kuonyesha uhodari wake katika kuwakumbua wachezaji wa timu ya taifa walioangamia.

Katika mechi ya pili ya robo fainali, Ivory Coast nao kwa idadi hiyohiyo ya mabao kama ya Zambia, yaani 3-0, iliwashinda wenyeji Equatorial Guinea, na ambao wamekuwa wakishirikiana na Gabon kuandaa mashindano ya mwaka huu.

Nahodha wa timu hiyo ya Elephants (Tembo), Didier Drogba, alikuwa mchezaji muhimu katika pambano la Jumamosi, licha ya kwamba mkwaju wa penalti katika kipindi cha kwanza uliokolewa na kipa Danilo. Lakini muda mfupi baadaye Drogba hakutaka kurudia kosa, na aliweza kufunga bao la kwanza, na katika kipindi cha pili, akaongezea bao la pili kwa kichwa.

Yaya Toure alipata bao la tatu, na kukamilisha kibarua hicho cha robo fainali. Ivory Coast imo katika kufanya juhudi za kulipata kombe hilo, ambalo limewaponyoka tangu mwaka 1992, na sasa watasafiri hadi Libreville, kumsubiri mshindi wa mechi nyingine ya robo fainali itakayochezwa Jumapili, kati ya wenyeji Gabon na Mali.
Nusu fainali zitachezwa siku ya Jumatano, tarehe 8 Februari.
-BBC