Zaidi ya yatima 1500 wanufaika na misaada ya Vodacom Foundation

Mkuu kitengo cha Vodacom Foundation, Yessaya Mwakifulefule akiwakabidhi baadhi ya watoto yatima mbuzi kwa niaba ya watoto wenzao wa mkoa wa Kigoma, wakati wa hafla fupi ya kufuturisha na kutoa misaada mbalimbali, kupitia kampeni ya Ramadhan Care & Share inaendeshwa na mfuko huo, wakati wa mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhan.

Kaimu Shekhe Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Shekhe Hassan Idd Hassan Kiburwa wa pili toka kulia pamoja na Mkuu wa kitengo cha Vodacom Foundation Yessaya Mwakifulefule (kulia)wakiwa wameshikilia madaftari tayari kwa kumkabidhi mtoto yatima na anaeishi katika mazingira magumu Zulpha Ally, wakati wa hafla fupi ya kufuturisha na kutoa misaada mbalimbali katika mkoa wa Kigoma, kupitia kampeni ya Ramadhan Care & Share mjini humo inaendeshwa na Vodacom Foundation, wakati wa mfungo huu wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhan, aliembeba mtoto huyo ni Meneja wa Mfuko huo Bi. Grace Lyon.

*Ni kuipitia kampeni ya Care and Share

ZAIDI ya watoto yatima 1500 wamenufaika na kampeni ya Care & Share mwaka huu, ikiwa ni mpango uliochini ya Vodacom Foundation.

Kampeni hiyo ambayo ilianzishwa mwaka 2007, imeshuhudia watoto yatima kutoka katika mikoa mitatu ya Tanga, Mtwara na Kigoma, wakipokea misaada mbalimbali katika kipindi cha mwezi mtukufu wa Ramadhan.

Akizungumza wakati wa kuhitimisha mpango wa Care and Share mkoani kigoma, Mkuu wa Kitengo cha Vodacom Foundation, Yessaya Mwakifulefule amesema kuwa kampeni ya mwaka huu imekuwa na mafanikio makubwa na imefikia maelfu ya watoto yatima.

“Tumetoa vyakula, vifaa vya kufundishia, mavazi na vifaa vingine kwa watoto yatima Waislamu kwa mwaka huu. Tunatambua kuwa Waislamu ni sehemu kubwa ya familia ya Vodacom Tanzania. Tukitambua kipindi hiki ni muhimu kwao, kwa kupitia mpango huu, tumeweza kuungana, kusheherekea na kubadilishana mawazo pamoja. Kwa miaka mitano sasa tumekuwa tukifanya hivi kusheherekea kwa pamoja kama sehemu ya familia,” alisema Mwakifulefule.

Kampeni hii ya Care & Share ni njia pekee ambayo Vodacom Foundation imekuwa ikitumia katika kushughulikia changamoto mbalimbali zinazo wakabili watoto yatima na vituo vyao.

Naye Kaimu Shekhe Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Shekhe Hassan Idd Hassan Kiburwa licha ya kuipongeza kampuni hiyo kwa kuanzisha mfuko wa kusaidia jamii alitoa wito kwa makampuni mengine kuiga mfano ya Vodacom kuwafikia watoto yatima hata pembezoni mwa Tanzania na siyo kung’ang’ania mijini tu.

“Naomba makampuni mengine hapa nchini kujitokeza kwa wingi na kwa moyo mkunjufu kabisa kwa kusaidia watoto yatima hapa nchini kwani wapo wengi na wanahitaji faraja toka kwetu sote,” alisisitiza Shekhe Kiburwa.

Kampeni hii ni sehemu ya shughuli mbalimbali na ofa ambazo kampuni imeanzisha ili kuwanufaisha waislamu kote nchini. Tangu kuanza kwa Mwezi mtukfu wa Ramadhan, wateja wa malipo ya kabla wameweza kufurahia ofa ya kupiga simu, kutuma ujumbe mfupi wa maneno na kutumia intanet bila kikomo kwa sh. 250 kwa siku.