Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete ameishukuru Kampuni ya Kimataifa ya Mbolea ya YARA International ASA kwa kuendelea kuunga mkono jitihada za Tanzania kuleta mageuzi katika kilimo nchini na kwa uamuzi wake wa kuifanya Tanzania kituo kikuu cha kikanda cha shughuli za kampuni hiyo ya kimataifa.
Aidha, Rais Kikwete amewaambia viongozi wa Kampuni hiyo kuwa Tanzania itahitaji mbolea nyingi mno katika siku za karibuni katika jitihada zinazofanyika sasa kuleta mageuzi makubwa katika kilimo kwa nia ya kujihakikishia usalama wa chakula na kuwaondoa wakulima katika umasikini.
Rais Kikwete ameyasema hayo leo, Jumatano, Juni 6, 2012 wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na ujumbe wa uongozi wa Kampuni hiyo Ikulu, mjini Dar es Salaam. Ujumbe huo wa watu 11 umeongozwa na Rais na Mtendaji Mkuu wa Kampuni hiyo yenye makao yake mjini Oslo, Norway, Bwana Jorgen Ole Haslestad.
Wengine katika ujumbe huo ni wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi – Bernt Reitan, Elisabeth Harstad, Geir O. Sundbo, Hilde Marete Aasheim, Guro Mauset, Juha Rantanen, Rune Bratterberg na Katibu wa Bodi hiyo Thor Giaaever. Pia walikuwemo Torgeir Kvidal ambaye ni Mkuu wa Manunuzi na Biashara na Sean de Cleene ambaye ni Mkuu wa Shughuli za Kimataifa, Mikakati na Maendeleo na Biashara.
YARA International ASA inawekeza katika ujenzi wa miundombinu maalum ya kupakua mbolea kwenye Bandari ya Dar es Salaam na ni miongoni mwa makampuni makubwa ya kimataifa yanayoshirikiana na Serikali ya Tanzania kuunga mkono miradi mkubwa ya kilimo.
Miradi hiyo ni pamoja ule wa Kuendeleza Kilimo katika Ukanda wa Kusini mwa Tanzania wa Southern Agricultural Growth Corridor of Tanzania – SAGCOT na ule wa kuendeleza kilimo katika Afrika wa Grow Africa.
Ujumbe huo wa YARA umekutana na Rais Kikwete baada ya kufanya ziara ya ukaguzi wa eneo la kilimo cha mpunga kwa kutumia mbinu za kisasa za umwagiliaji huko Dakawa, Morogoro ambako kampuni hiyo inashirikiana na Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Marekani (USAID) kuendeleza kilimo cha mpunga cha umwagiliaji katika eneo hilo.
Bodi hiyo pia itafanya kikao chake cha Bodi mjini Dar es Salaam kesho ikiwa ni mara ya kwanza kwa Bodi hiyo kukutana nchini na pia ikiwa ishara ya imani kubwa ya YARA katika uchumi wa Tanzania na kuthibitisha dhamira ya kampuni hiyo kuendelea kuwekeza nchini.
Wakati wa mazungumzo hayo, Bwana Jorgen Ole Haslestad amemshukuru na kumpongeza Rais Kikwete kwa kuonyesha uongozi na njia katika jitihada za kuleta mageuzi katika kilimo cha Tanzania na Afrika kwa jumla.