Na Mwandishi Wetu
TIMU ya Yanga ya Dar es Salaam imekamilisha mchezo wake wa mwisho wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara kwa kuibanjua Timu ya Simba magoli 2-0 bila kujali machungu ilionayo timu hiyo kwa kukosa ubingwa wa ligi hiyo kwa mwaka huu.
Mchezo huo uliovuta hisia za mashabiki na wapenzi wa mpira wa miguu kwa kiasi kikubwa leo umehudhuriwa na idadi kubwa ya watazamaji, ambapo inakadiriwa kuingiza zaidi ya watazamaji 60,000 walioingia kuzishuhudia timu hizo.
Yanga ndiyo waliokuwa na bahati ya mapema katika mchezo huo ya kupata goli, kwani iliwachukua dakika 4 tu tangu kuanza kwa mchezo huo kabla ya kujipatia bao la kwanza, mfungaji akiwa Kavumbagu aliyepokea pasi kutoka kwa Simon Msuva.
Katika dakika 18 Simba ilipata penati baada ya mchezaji wa Yanga Canavaro kumuangusha mchezaji hatari wa Simba Mrisho Ngassa eneo hatari, lakini kama waswahili wasemavyo siku ya kufa nyani miti yote uteleza, Musa Mudde alikosa penati hiyo.
Yanga ilifanikiwa kujipatia bao la pili katika dakika 62 ambapo Hamis Kiiza alipachika bao hilo baada ya kumfikia mpira wa kurushwa toka kwa mchezaji mwenzake, Mbuyu Twite.
Yanga ambao walikuwa tayari wametangaza ubingwa tangu awali kabla ya michezo yake ya mwisho, imekabidhiwa kikombe chake cha Ubingwa wa Ligi Kuu wa mwaka huu pamoja na kitita cha sh milioni 70. Hadi dakika 90 za mchezo huo zikimalizika Yanga 2 na Simba 0.
Simba katika mchezo huo iliwakilishwa na Juma Kaseja, Nassoro Masoud, Shamte Ramadhan, Shomari Kapombe, Musa Mudde, William Lucian, Mwinyi Kazimoto, Abdallah Seseme, Mrisho Ngassa, Amri Kiemba na Haruna Chanongo.
Yanga: Ally Mustafa, Mbuyu Twite, David Luhende, Nadir Haroub, Kelvin Yondan, Athuman Idd, Simon Msuva, Franka Damayo, Didier Kavumbagu, Hamis Kiiza na Haruna Niyonzima.