Timu ya Yanga SC imelazimishwa sare ya kufungana bao 1-1 na Al Ahly ya Misri katika mchezo wa kwanza hatua ya 16 Bora Ligi ya Mabingwa Afrika jioni ya leo Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Kwa matokeo, Yanga italazimika kwenda kushinda ugenini ili kutimiza ndoto za kucheza hatua ya makundi ya michuano hiyo kwa mara ya pili katika historia yao baada ya mwaka 1998.
Katika mchezo wa leo, mabao yote yalipatikana kipindi cha kwanza, Ahly wakitangulia kufunga kupitia kwa mshambuliaji wake mjanja, Amr Gamal, kabla ya Yanga kusawazisha kwa bao la ‘ngekewa’ la Issoufou Boubacar.
Gamal alifunga kwa kichwa akimalizia mpira wa adhabu uliopigwa na Ramadan Sobhi dakika ya 10, ambao uliwapita mabeki wote wa Yanga na kipa wao, Ally Mustafa ‘Barthez’ na kumkuta mfungaji pembeni ya lango akaujaza nyavuni.
Yanga walitulia baada ya baada ya bao hilo na kuanza kupanga mashambulizi yao vizuri, hatimaye kufanikiwa kupata bao la kusawazisha dakika ya 18 kupitia kiungo wa Niger, Boubacar.
Timu hizo zinatarajiwa kurudiana Aprili 19 mjini Cairo na mshindi wa jumla atafuzu hatua ya makundi, wakati timu itakayotolewa itaangukia kwenye kapu la kuwania kucheza hatua ya makundi kombe la Shirikisho.
Chanzo: Bin zubeiry.co.tz