Yanga Yapigwa Faini ya Mil 20 kwa Vurugu, Simba Nayo Mil 5

Yanga Yapigwa Faini ya Mil 20 kwa Vurugu, Simba Nayo Mil 5

Yanga Yapigwa Faini ya Mil 20 kwa Vurugu, Simba Nayo Mil 5


 
KLABU za Yanga na Simba zimeagizwa kulipa jumla ya sh. milioni 25 kutokana na uharibifu wa viti na vurugu zilizofanywa na washabiki wao kwenye mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kati ya Yanga na Al Ahly ya Misri iliyochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
 
Yanga italipa sh. milioni 15 ambayo ni gharama ya uharibifu wa viti uliofanywa na washabiki kwenye mechi hiyo. Pia imepigwa faini ya sh. milioni tano kutokana na vurugu za washabiki wake. Nayo Simba imepigwa faini ya sh. milioni tano kutokana na washabiki wake kuhusika katika vurugu hizo.
Uamuzi huo umefanywa na Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) katika kikao chake cha dharura kilichofanyika jana (Machi 19 mwaka huu) jijini Dar es Salaam.
 
Tunatoa onyo kwa washabiki wa mpira wa miguu kujiepusha na vurugu viwanjani ikiwemo uharibifu wa miundombinu mbalimbali ya viwanja ikiwepo viti, na tutachukua hatua kali zaidi kwa klabu na washabiki wake iwapo vitendo hivyo vitajitokeza tena.
 
RWIZA, LIUNDA KUSIMAMIA MECHI ZA CAF
Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) limewateua Watanzania Alfred Rwiza na Leslie Liunda kusimamia mechi zake za wikiendi hii na mwezi ujao.
 
Liunda ameteuliwa kuwa Kamishna wa mechi ya Kombe la Shirikisho (CC) kati ya How Mine ya Zimbabwe na Bayelsa United ya Nigeria itakayochezwa Jumamosi (Machi 22 mwaka huu) jijini Bulawayo.
 
Waamuzi wa mechi hiyo wanatoka Eritrea, na wanaongozwa na Maeruf Kherseed. Wasaidizi wake ni Angeson Ogbamariam, Berhe O’Michael na Luelseghed Ghebremichael.
 
Naye Rwiza atasimamia mechi ya michuano ya Afrika kwa vijana wenye umri chini ya miaka 20 kati ya Lesotho na Swaziland itakayochezwa kati ya Aprili 25-27 mwaka huu jijini Maseru.
 
Mechi hiyo ya marudiano itachezwa na waamuzi Duncan Lengani, Innocent Kaundula, Hendrix Maseko na Jones Makhuwira, wote kutoka nchini Malawi.