Yanga Yang’ara, Azam Wabaniwa Tena

yanga

YANGA SC imejiimarisha kidogo kwenye mbio za ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara baada ya ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya wenyeji, Toto Africans Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.

Kwa ushindi huo uliotokana na mabao ya Mzambia Obrey Chirwa na mzawa Simon Msuva, Yanga inafikisha pointi 18 baada ya kucheza mechi tisa ingawa inaendelea kukamata nafasi ya tatu, nyuma ya Stand United na Simba.

Katika mchezo huo uliochezeshwa na Andrew Shamba wa Pwani, Yanga ilimaliza dakika 45 za kipindi cha kwanza ikiwa inaongoza kwa bao 1-0, lililofungwa na mshambuliaji Mzambia, Obrey Chirwa aliyemalizia kwa kichwa krosi ya Simon Msuva dakika ya 29.

Safu ya ulinzi ya Yanga nayo ilipewa misukosuko kidogo na washambuliaji chipukizi wa Toto, Waziri Junior na Reliant Lusajo.

Kipindi cha pili, Yanga walirejea vizuri tena na kuendelea kuutawala mchezo. Haikushangaza winga Simon Msuva alipofunga bao la pili kwa penalti baada ya Kaseke kuangushwa kwenye boksi.

Matokeo Mengine

Ndanda FC 1 vs 1 Mbeya City
Ruvu Shooting1 vs 1 Mwadui FC
African Lyon 1 vs 2 Majimaji FC
Tanzania Prisons 2 vs 1Stand United
Azam 1 Kagera 1

Chanzo:binzubeiry.co.tz