YANGA SC imefufua matumaini ya kwenda Nusu Fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika, kufuatia ushindi wa 1-0 jioni ya leo dhidi ya Mouloudia Olympique Bejaia ya Algeria katika mchezo wa marudiano Kundi A Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Shukrani kwake, mshambuliaji wa kimataifa wa Burundi, Amissi Josleyn Tambwe aliyefunga bao hilo pekee mapema tu kipindi cha kwanza.
Ushindi huo wa kwanza baada ya mechi tano, unaifanya Yanga ifikishe pointi nne baada ya awali kufungwa mechi tatu na kutoa sare moja ingawa inaendelea kushika mkia katika Kundi A.
Mazembe inaongoza Kundi A kwa pointi zake 10 baada ya mechi nne, ikishinda tatu na kutoa sare moja, ikifuatiwa na Bejaia na Medeama, ambazo kila moja ina pointi tano za sare tatu na ushindi mmoja.
Tambwe alifunga bao hilo dakika ya pili tu ya mchezo, akimalizia mpira uliookolewa kufuatia Simon Msuva kuunganisha kwa kichwa krosi ya Juma Abdul kutoka upande wa kulia.
Yanga sasa inaomba Medeama ya Ghana ifungwe na TP Mazembe kesho na baadaye ikatoea sare na MO Bejaia ili kwenda Nusu Fainali.
Yanga ingeweza kuondoka na ushindi mnono leo, kama mshambuliaji wake, Obrey Chirwa angekuwa makini na kutumia vizuri nafasi zaidi ya nne za wazi alizotengenezewa.
Nafasi iliyowasikitisha zaidi mashabiki wa Yanga ni ya kipindi cha pili, Chirwa aliporuka kichwa cha mkizi baada ya krosi ya Simon Msuva kutoka kushoto, lakini akapiga hewa akiwa amebaki na kipa, huku mpira ukienda nje.
Kocha Mholanzi, Hans van der Pluijm alilazimika kufanya mabadiliko ndani ya robo ya kwanza ya mchezo, baada ya beki wake, Andrew Vincent ‘Dante’ kuumia na kumuingiza mkongwe, Kevin Yondan aliyemalizia vizuri mchezo.
Na akalazimika pia kumpumzisha beki wake wa kulia, Juma Abdul baada ya kipindi cha kwanza kufuatia kuumia nyama na kumuingiza kiungo Said Juma ‘Makapu’ aliyekwenda kucheza kama kiungo ea ulinzi, huku Mbuyu Twite akihamia beki ya kulia.
Yanga itahitimisha mechi zake za Kundi A Kombe la Shirikisho kwa kumenyana na wenyeji TP Mazembe ya DRC mjini Lubumbashi Agosti 23, mwaka huu.
Chanzo:binzubeiry.co.tz