Na; binzubeiry.co.tz
YANGA SC inapanda ndege leo kwenda Kigali, Rwanda kwa ajili ya mchezo wa kwanza wa Raundi ya Kwanza, Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya wenyeji, APR Jumamosi.
Yanga SC itashuka Uwanja wa Amahoro, Kigali, Rwanda Jumamosi ikiwa na kumbukumbu ya kufungwa mabao 3-0 mjini humo walipokutana mara ya kwanza na ya mwisho kwenye michuano mwaka 1996.
Timu ya jeshi la Rwanda, nchi inayoongozwa na Rais Paul Kagame iliitoa Yanga katika Raundi ya Kwanza ya Ligi ya Mabingwa mwaka 1996 jumla ya mabao 3-1, ikishinda 3-0 Kigali kabla ya kuja kufungwa 1-0 Dar es Salaam.
Miaka 20 baadaye, timu hizo zinakutana tena katika hatua ile ile – na michuano ile ile, tena kwa namna ile ile, Yanga wakianzia ugenini.
Kocha Mholanzi wa Yanga SC, Hans van der Pluijm amesema kwamba wanakwenda kwenye mchezo mgumu wa ugenini dhidi ya APR, lakini watapambana wasipoteze.
Pluijm amesema kwamba mchezo huo wa kwanza wa Raundi ya Kwanza Ligi ya Mabingwa Afrika, utakuwa mgumu kwa sababu APR ni timu nzuri.
“APR ni timu nzuri na watakuwa wamejiandaa vizuri, lakini sisi tuko vizuri, tutakwenda kupambana tusipoteze mchezo, ili tumalizie vizuri mchezo wa nyumbani,”amesema.
Kwa upande wake, kocha mpya wa APR, Nizar Khanfir amesema kwamba amewaona Yanga katika video na anataka kuwafunga Jumamosi.
“Lengo letu ni kushinda huo mchezo”amesema na kuongeza; “Nimeona baadhi ya video zao na tutaendelea kuwachambua katika siku chache zijazo kuelekea kwenye mechi,”.
Mechi hiyo inatarajiwa kuchezeshwa na marefa wa Malawi Jumamosi Uwanja wa Amahoro, Kigali Rwanda.
Duncan Lengani anatarajiwa kupuliza filimbi, wakati washika vibendera watakuwa Clemence Kanduku na Jonizio Luwizi.
Mchezo wa marudiano wiki moja baadaye Dar es Salaam, utachezeshwa na marefa wa Shelisheli; katiati Bernard Camille na pemebeni watakuwapo Eldrick Adelaide na Gerard Pool