Yanga Yaipumulia Simba, Azamu Azidi Kuchanja Mbuga

yanga

YANGA SC imezinduka katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, baada ya kuichapa Maji Maji ya Songea mabao 3-0 jioni ya leo Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.

Mfungaji bora wa Ligi Kuu msimu uliopita, Amissi Joselyn Tambwe alifunga mabao mawili kipindi cha pili baada ya kiungo Deus David Kaseke kutangulia kufunga kipindi cha kwanza.

Yanga sasa inafikisha pointi saba, baada ya kucheza mecni tatu, ikishinda mbili na sare moja – sawa na mahasimu wao, Simba SC.
Winga Simon Msuva hakuwa mwenye bahati leo, baada ya kupoteza nafasi kadhaa za kufunga mabao, ikiwemo penalti.

Msuva alipiga penalti mbili zote akafunga, lakini refa akamuamuru kurudia, ya kwanza akidaiwa kutishia kabla ya kupiga na ya pili, refa akisema wachezaji wenzake walisogea kabla hajapiga.

Msuva alipokwenda kupiga kwa mara yatatu, mpira ukagonga mwamba na kurudi uwanjani kabla ya kutokea piga nikupige na kumkuta Kaseka aliyefunga dakika ya 19.

Tambwe akaifungia Yanga bao la pili kwa kichwa akimalizia pasi ya Simon Msuva kufuatia krosi ya Juma Mahadhi. Tambwe akafunga bao la tatu akimalizia krosi ya Mahadhi tena.

Mechi nyingine za Ligi Kuu leo, Mwadui FC imelazimishwa sare ya 2-2 na ndugu zao Stand United Uwanja wa Mwadui Complex, Shinyanga, Mbeya City imefungwa nyumbani 2-1 na Azam FC na Ndanda FC imelazimishwa sare ya 0-0 na Kagera Sugar, Ruvu Shooting imewalza ndugu zao JKT Ruvu 1-0 Uwanja wa Mabatini, Mlandizi Pwani.

Matokeo ya mechi nyingine
Mbeya City 1-2 Azam
Ruvu Shooting 1-0 JKT Ruvu
Mwadui FC 2-2 Stand Unied
Ndanda FC 0-0 Kagera Sugar

Chanzo:binzubeiry.co.tz