Yanga yaendelea kuumia, yatakiwa kulipa tena mil 5

Baadhi ya wachezaji wa timu ya Yanga ya Dar es Salaam

Na Mwandishi Wetu

SAKATA la vurugu za mashabiki wa Yanga kati ya mchezo wake na timu ya Azam, limeendelea kuigharimu timu hiyo na sasa imetakiwa kulipa sh. milioni tano ikiwa ni fidia ya uharibifu wa viti uliofanywa na mashabiki hao.

Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) leo, Machi 14, 2012 limepokea barua kutoka Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo juu uharibifu uliofanyika kutokana na vurugu za washabiki wa Yanga kwenye mechi dhidi ya Azam.

Kwa mujibu wa tathmini ya Serikali, katika vurugu hizo kwenye mechi hiyo ya Ligi Kuu ya Vodacom iliyochezwa Machi 10 mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam jumla ya viti 119 viliharibiwa. Gharama za uharibifu huo ni sh. milioni 5 ambazo Serikali imeagiza zilipwe mara moja.

Kwa vile washabiki wa Yanga ndiyo waliohusika na vurugu na uharibifu huo, gharama hizo zitabebwa na klabu hiyo ili Serikali iweze kufanya ukarabati haraka.

TFF inarudia tena kulaani na kukemea vurugu zinazofanywa na washabiki viwanjani na kusababisha usumbufu, uvunjifu wa amani na uharibifu wa vifaa hasa kutokana na ukweli kuwa mpira wa miguu ni mchezo wa burudani.

Tunapenda kuwakumbusha washabiki na klabu kuwa vitendo hivyo si vya kistaarabu, hivyo havikubaliki katika mpira wa miguu, na TFF haitasita kuchukua hatua kali kwa wahusika iwapo vitaendelea kutokea viwanjani.

Wakati huo huo; Rais wa TFF, Leodegar Tenga kesho, Machi 15 mwaka huu atakuwa na mkutano na waandishi wa habari. Mkutano ambao utafanyika saa 6 kamili mchana kwenye ofisi za TFF, Karume jijini Dar es Salaam.