Yanga watafuata nyayo za Simba leo?

Dar es Salaam

MABINGWA wa Soka Tanzania Bara, Yanga leo wanajitupa uwanjani kuvaana na St. Gearge katika mchezo wa hatua ya Nusu Fainali ya Michuano ya Kagame Cup mchezo utakaofanyika kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Mchezo huo unaotabiriwa kuwa mkali kutokana na kila timu kutaka kuingia hatua ya fainali ili iweze kuibuka bingwa na kunyakuwa kitita cha dola 30,000 ambazo zinatolewa na mdhamini wa mashindano hayo Rais wa Rwanda, Poul Kagame. Tayari Simba imeingia fainali baada ya kuitoa El Mereikh jana kwa penati na inamsubiri mshindi wa leo.

St. George iliyoingia katika hatua hiyo bila ya kupoteza mchezo haya mmoja katika hatua ya awali na hatua ya robo fainali inakibarua kigumu dhidi ya wanajangwani hao ambao watakuwa kwenye Uwanja wao wa nyumbani. Endapo St. George itaendeleza wimbi lake la ushindi itakuwa imeiondoa Yanga katika hatua ya kucheza fainali hiyo na kusubili kucheza kuwania nafasi ya mshindi wa tatu.

Yanga inaingia uwanjani ikijivunia wachezaji wake wa kigeni kama vile Keneth Asamoah, Davies Mwape, Hamis Kiiza na Yaw Berko ambao waameonekana kuwa kivutio kikubwa kwa Yanga kwa kuweza kumudu vizuri nafasi zao.

Wachezaji hao wamekuwa wakitoa mchango mkubwa kwa timu yao kila mara inapokuwa na mchezo katika mashindano haya. Timu itakayoshinda mchezo huo itavaana na timu ya Simba, ambayo iliitoa El Mereikh, ambayo sasa inamgoja atakayefungwa leo kupambana kuwania nafasi ya mshindi wa tatu.