Na Mwandishi Wetu
WANACHAMA wa klabu ya Yanga tawi la Tabata wametakiwa kujitokeza kwa wingi katika mkutano wa mwaka utakaofanyika kesho, Jumatatu (26 Desemba, 2011) kwenye Ukumbi wa Ofisa Mtendaji Kata huku ajenda kubwa ikiwa ni maandalizi ya mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya Bara.
Akizungumza jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu wa tawi hilo, Michael Warioba alisema, wanachama wa tawi hilo wanatakiwa kujitokeza kwa wingi kushiriki mkutano huo utakaoudhuriwa na vingozi wa kitaifa wa timu hiyo.
“Vitu vingi tutavizungumzia kama vilivyoorodheshwa katika ajenda zetu, lakini kubwa ni maandalizi ya timu katika mzunguko wa pili wa ligi kuu, pia mchezo wetu na Zamalekh (Kombe la Shirikisho Afrika).
“Tunaomba wanachama wajitokeze kwa wingi saa 4:00 asubuhi katika mkutano huo ili tuweze kuijenga klabu yetu na kutetea ubingwa wa Bara,” alisema Warioba.
Pia Warioba amewataka wapenzi wa klabu hiyo kujitokeza kuchukua kadi za uanachama wa Yanga ili waweze kupata nafasi ya kutoa mchango wa hali na mali katika kuhakikisha timu inafanya vizuri kwenye michuano mbalimbali.