Yanga, Simba uso kwa uso fainali ya Kagame leo


Na Joachim Mushi

TIMU ya Yanga ya Dar es Salaam ambao pia ni mabingwa wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara wanatarajia kupanda uwanjani kupepetana na watani wao wa jadi Simba ya Dar es Salaam.

Mchezo huo wa Fainali ya Kombe la Kagame unatarajia kuwa mgumu kwa pande zote kutokana na uhasimu wa soka uliopo kati ya timu zote mbili, ambazo mara zote zimekuwa na ushindani mkubwa kila zinapokutana.

Simba ambayo iliingia Fainali ya Kagame baada ya kuitoa timu ya El Mereikh kwa penati 5-4, baada ya kucheza dakika 120 bila kupatikana mshindi kwenye mchezo wa nusu fainali ya kombe hilo, imekuwa ikijinasibu kushinda mchezo huo dhidi ya mtani wake.

Yanga nayo ilifanikiwa kuingia fainali kama ilivyokuwa kwa Simba, kwani ilicheza dakika 120 na timu ya St. George bila kupatikana mbabe, ambapo mwamuzi aliamuru zipigwe penati ndipo yanga ilipofanikiwa kuitoa timu hiyo.

Mchezo huo ambao utatangulia na mchezo kati ya St. George na El Mereikh kutafuta mshindi wa tatu, unatarajiwa kuchezwa leo jioni katika Uwanja wa Taifa wa Dar es Salaam.

Hata hivyo matokeo yoyote ya mchezo wa pili kati ya Simba na Yanga yatakuwa mazuri kwa Watanzania na haswa Shirikisho la Soka nchini (TFF), ambalo lilizihimiza klabu za Simba na Yanga kuhakikisha zinafanya vizuri ili kombe libaki Tanzania, jamba ambalo limefanikiwa.