Yanga Mwendo Mdundo VPL Yachinja Mtu Taifa 5-0

Nembo ya Timu ya Yanga

Habari na bioplus.blogspot.com
MABINGWA wa soka Tanzania bara, Yanga leo wamefanikiwa kurejea kileleni mwa ligi kuu ya Vodacom na kuwashusha mahasimu wao Simba hadi nafasi ya pili baada ya kuwatandika African Sports ya Tanga mabao 5-0, katika mchezo uliochezwa kwenye dimba la Taifa jijini Dar es Salaam.

Mchezo huo ulianza kwa Yanga kuliandama lango la Sports lakini vijana hao wa Tanga walionekana kutulia na kuharibu mipango yote ya mabingwa hao watetezi waliokuwa wakionekana wazi kupania kurejea kileleni kabla hawajaanza safari ya Rwanda wanakoifuata APR ya jijini Kigali katika mchezo wa ligi ya mabingwa Afrika.

Katika dakika ya 32, mpira uliookolewa na mabeki wa Sports ulimkuta Kevin Yondan akiwa nje kidogo ya eneo la 18 ambaye alifumua shuti kali lililowababatiza mabeki na kutinga nyavuni. Kipa wa Sports Kabali Faraji hakuwa na la kufanya kwavile mpira huo ulibadili uelekeo hivyo kushtuka amepelekwa ‘sokoni’.

Bao la pili la Yanga lilifungwa na Mzimbabwe Donald Ngoma kwa mtindo wa ‘kibaiskeli’ akimalizia krosi ya beki aliyeonyesha kiwango cha juu hivi karibu, Juma Abdul ambaye alipanda na mpira hafi karibu na eneo la kibendera kabla hajamimina krosi hiyo.

Kipindi cha pili Yanga waliongeza kasi ya mashambulizi ambapo katika dakika ya 51, Amissi Tambwe aliweka nyavuni mpira ambao ulimkuta baada ya kuokolewa na kipa Kabali kufuatia krosi ndefu ya Haruna Niyonzima. Hata hivyo wachezaji wa Sports walilalamikia bao hilo wakidai mfungaji aliunawa mpira kabla hajafunga.

Matheo Anthony aliiandikia Yanga bao la nne kwa kichwa katika dakika ya 59 ukiwa ni mpira wake wa kwanza kuugusa tangu achukue nafasi ya Ngoma. Bao hilo lilitokana na kross ya beki wa kushoto Haji Mwinyi.

yanga

Dakika ya 72, Tambwe aliifungia Yanga bao la tano na kufikisha mabao 17 akimzidi Hamis Kiiza wa Simba kwa bao moja.

Kwa ushindi huo Yanga wamerejea kileleni mwa ligi wakiwa na pointi 50 wakifuatiwa na Simba yenye pointi 48 huku Azam ikishika nafasi ya tatu kwa kujikusanyia pointi 47