BAADA ya timu ya Yanga ya Dar es Salaam kutangazwa Mabingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, hali imekuwa mbaya kwa wapinzani wao wa jadi timu ya Simba na sasa wameanza kutimuana.
Yanga na Simba wameringana pointi yaani wote wamefikisha pointi 46 kila mmoja ila Simba amefungwa magoli 17 huku Yanga akifungwa magoli 7 tu, sehemu ambapo amemzidi mpinzani wake.
Simba imeamua kulifumua upya benchi la ufundi na kuwaondoa wachezaji 15 katika orodha ya usajili wa Ligi Kuu ya Tanzania.
Akizungumza Dar es Salaam jana mmoja wa viongozi waandamizi wa klabu ya Simba, amesema klabu hiyo imeona bora ifanye hivyo ili kuinusuru timu hiyo.
Kiongozi huyo ameongeza kuwa kuna vitu vingi amevigundua kama baadhi ya wachezaji kujiamini na kufanya kila wanachotaka kwa faida zao huku wakiiumiza timu.
Alisema baada ya kuangalia kwa kina wamelibaini hilo hivyo kuamua wawaache watafute timu nyingine za kucheza. “Nimegundua kuna watu wapo kwa ajili ya maslai yao na si timu hiyo ni bora tuwaache wafanye mambo yao na kwenda kuchezea timu wanazotaka wao,” alisema kiongozi huyo wa simba.
Alisema kuna baadhi ya wachezaji wamekuwa wakifanya vitu tofauti na mikataba yao na bila ya kutambua kuwa mpira ndiyo maisha kwao.
“Tunavunja mikataba ya wachezaji wanne ambao walikuwa bado mwaka mmoja hii yote tuiweke timu sawa…na kuondoa kirusi kilichopo ndani ya timu inaaelekea kila msimu tutaendelea kufanya hivi hivi kama tutaendelea kuwa nao,” alisema.
Hata hivyo chanzo kingine cha habari kinasema baadhi ya wachezaji wanaoachwa yumo mchezaji mkongwe wa timu hiyo, Mussa Hassan Mgosi, Kelvin Yondani na Mohamed Banka.