Yamoto Band, FM Academia, Sylight na Mapacha Jukwaa Moja…!

Yamoto Bandi

Yamoto Bandi

Na Mwandishi Wetu

BENDI nne nyota nchini, FM Academia, Yamoto, Mapacha na SkyLight zitatumbuiza katika jukwaa moja kwenye tamasha la Beach band Bonanza lililopangwa kufanyika Desemba 20 kwenye ufukwe wa Azura, Kawe darajani.

Bonanza hilo limeandaliwa na kampuni ya Team Mamba na mbali ya bendi hizo nyota, wasanii wa bongo fleva wakiongozwa na Dully Sykes, CPWAA na Damian Soul ambaye atakuja na bendi yake.

Msemaji wa kampuni ya Team Mamba, Doris Godfrey alisema kuwa bonanza hilo lililodhaminiwa Coca-Cola na bia ya Windhoek, limepangwa kuanza saa 6 mchana mpaka alfajiri. Doris alisema kuwa wameandaa bonanza hilo kwa ajili ya kuwakutanisha wadau wa muziki na familia zao kwani siku hiyo kutakuwa na michezo ya watoto mchana na baadaye usiku kwa ajili ya wakubwa.

Alisema kuwa pia kutakuwa na michezo ya watoto, kupanda farasi na michezo mingine ambayo ni ya kuvutia. “Hili ni bonanza la kwanza la muziki linalokutanisha bendi nyingi ambazo zitafanya shoo katika jukwaa moja, hivyo tunatarajia kuwa na burudani aina yake kwani bongo fleva nao watakuwepo kwa lengo kutoa burudani safi,” alisema Doris.

Kiongozi wa bendi ya FM Academia, Nyoshi El Sadaat alisema kuwa wamejiandaa vizuri kutoa burudani katika bonanza hilo la aina yake. “Tuna nyimbo mbalimbali mpya, staili mpya ambazo siku hiyo zitakuwa zinaonyeshwa mara kwanza jukwaani,” alisema Nyoshi.

Kwa upande wake, Dully Sykes alisema kuwa wamejiandaa vilivyo kwa ajili ya tamasha hilo na kuwaomba mashabiki wa muziki kufika kwa wingi.