Na Mwandishi Wetu Ruvuma
SHIRIKA la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO) lilianzishwa kwa Sheria ya Bunge Namba 28 ya mwaka 1973. Shirika lilianzishwa kwa malengo ya kupanga, kuratibu na kutoa huduma zitakazosaidia kuendeleza ustawi wa viwanda na biashara ndogo nchini.
Shirika hilo limekuwa likihusika na kutoa huduma za kuendeleza teknolojia, kutoa mafunzo kwa ujasiriamali na ugani, masoko, habari na fedha. Katika Mkoa wa Ruvuma, shirika lilianza shughuli zake mwaka 1974 na baadaye kuanzisha Mtaa wa Viwanda kwa kufungua ofisi mwaka 1976.
Miongoni mwa sababu zilizopelekea kuanzishwa kwa SIDO ni kuhakikisha kuwa rasilimali zilizo ndani ya nchi zinatumika ipasavyo kukidhi mahitaji ya ndani, lakini pia kupunguza utegemezi wa kuagiza kila bidhaa nje ya nchi.
MAFANIKIO
Baadhi ya mafanikio ambayo yamepatikana katika Mkoa wa Ruvuma kupitia Shirika la SIDO katika miaka 50 ya uhuru ni kupiga hatua katika teknolojia ambazo zinahitajika katika maeneo ya mkoa hususan teknolojia zinazosaidia wakulima, viwanda na matumizi ya nyumbani.
Tenkolojia zilizoweza kupatikana na kusambazwa katika Mkoa wa Ruvuma ni pamoja na teknolojia ya utengenezaji wa chaki, usindikaji ngozi, utengenezaji wa sabuni za aina mbalimbali, matumizi ya nguvu za maji katika kuendesha mashine za kusaga nafaka na kuzalisha umeme, ubanguaji korosho na uundaji wa zana za kufanyia kazi za mikono kwa mafundi wadogo.
Kuhusiana na uundaji wa mashine, sasa hivi katika Mtaa wa Viwanda wa SIDO uliopo Songea na maeneo ya wajasiriamali binafsi, mashine za aina mbalimbali zinapatikana. Mfano, mashine za kupukuchua mahindi, kusaga na kukoboa nafaka, kukoboa kahawa, kuranda, kupasulia mbao na magogo, kubangua karanga pamoja na kukamua juisi ya miwa.
Mafundi wadogo wasiopungua 1,250 wamesaidiwa katika kupatiwa mafunzo na msaada wa vitendea kazi kwa kushirikiana na shirika lisilo la kiserikali la Uingereza (TFSR) na pia huduma ya masoko.
Kaimu Meneja wa SIDO Ruvuma, Athur Ndedya, anasema kwamba katika kupunguza tatizo la uhaba wa maeneo ya kufanyia kazi, wameazimia kuongeza majengo 16 katika mtaa wa viwanda na pia kutafuta pesa kwa ajili ya kujenga eneo lingine lenye ukubwa wa mita 6,065 za mraba kwa ajili ya mafundi wa fani za useremala na uchomeleaji katika manispaa ya Songea.
“Katika jitihada za kuwasaidia wajasiriamali kukabiliana na changamoto ya upatikanaji wa mitaji kwa ajili ya kuendeshea shughuli zao, shirika limetoa mikopo 2,184 yenye thamani ya sh. bilioni 3.5 kupitia mfuko wa taifa wa kuendeleza wajasiriamali nchini na mfuko wa mkoa. Katika mikopo hii vikundi 84 vyenye thamani ya zaidi sh. milioni 308 ilitolewa vijijini kwa wananchi 2,512”.
Ndedya anasema kupitia Programu ya Fanikiwa Kibiashara inayohusisha shindano na mafunzo ya kuandika michanganuo ya biashara inayoendeshwa na SIDO, wajasiriamali wasiopungua 246 wamefaidika kwa kupata sh. milioni 610 ikiwa ni ruzuku ya kuendeleza miradi yao.
HUDUMA YA MAFUNZO, USHAURI NA MASOKO
Katika jithada za kuwasaidia wajasiriamali katika eneo la masoko shirika limeanzisha kituo cha habari kwa njia ya mtandao na pia kituo cha kuonyesha teknolojia na bidhaa za wajasiriamali.
Ndedya anasema lengo la kituo ni kuwasaidia wajasiriamali kutoa na kupata taarifa za masoko, malighafi na bidhaa zao lakini pia kupata taarifa juu ya huduma mbalimbali zinazohusu wajasirimali zinazotolewa na taasisi mbalimbali zilizo nje ya mkoa wa Ruvuma. Pia kituo kinatoa mafunzo ya kumpyuta kwa wajasiriamali.
“Katika jitihada za kutangaza bidhaa zinazozalishwa na wajasiriamali katika maeneo yetu tumeweza kuandaa maonyesho mara sita kikanda ambayo yamehusisha wajasiriamali 1,611 toka mikoa mbalimbali na Kenya, yaliyopesaidia wajasiriamali kupata oda na mauzo zaidi ya sh. milioni 394. Katika mkoa wa Ruvuma kuna wajasiriamali wapatao saba ambao tayari bidhaa zao zimethibitishwa na Shirika la Viwango vya Ubora ( TBS).
“Tumefanikiwa kutoa mafunzo kwa wajasiriamali wengi katika mafunzo ya ujasiriamali, mafunzo ya ujuzi kama vile utengenezaji chaki , sabuni, batiki, usindikaji wa vyakula na matunda, uandishi wa michanganuo ya miradi na mafunzo ya kuboresha bidhaa kwa mafundi wadogo na mafunzo haya yamesaidia uanzishwaji wa viwanda vidogo vinavyojishughulisha na taaluma tajwa,”anasema.
CHANGAMOTO
Changamoto kubwa ambayo sekta ya viwanda vidogo inakabiliana nayo ni mfumo wa soko huria pamoja na utandawazi, ambapo wajasiriamali wadogo wanalazimika kuingia kweye ushindani na viwanda vikubwa vilivyopo ndani na nje ya nchi.
Ndedya anasema kuna mwamko mdogo wa Watanzania kuwekeza katika shughuli za uzalishaji licha ya kuwa na ushindani mdogo ukilinganisha na biashara za uchuuzi ambazo zimekuwa ndio kimbilio la wengi na wakati mwingine kukosekana kwa taasisi nyingi ambazo ziko tayari kusaidia miradi ya uwekezaji na uzalishaji ambayo huchukua muda mrefu kabla ya kuanza kutoa faida.
MATARAJIO
“Malengo yetu ni kuhakikisha tunaongeza kasi ya kuwa na viwanda vidogo katika maeneo ya vijijini. Kipaumbele kitakuwa ni viwanda vya kuongeza thamani ya mazao kwa lengo la kuwafanya wakulima wapunguze uuzaji wa mazao ghafi na pale wanapouza wauze kwa tija. Kwa mkoa wa Ruvuma tutaangalia mazao ya alizeti , korosho na mhogo pamoja na mazao mengine kulingana na mahitaji ya wananchi.
“Katika jitihada za kuwasaidia wajasiriamali kukabiliana na changamoto wanazokutana nazo na kuhakikisha zinapatiwa ufumbuzi, tunalenga kushirikisha wadau wengi zaidi ambao wanatoa huduma zinazohitajika katika kuendeleza viwanda na biashara ndogo,”anasema.
Pia, anasema wanatarajia kubadili mtazamo wa wananchi kwa kutoa elimu ya ujasiriamali ili kuongeza ubunifu na kuchochea chachu ya uendelezaji biashara kwani wananchi bado hawajaweza kutumia fursa mbalimbali zilizopo nchini na nchi jirani za Msumbiji na Malawi kwa kukuza uchumi wa mkoa.
Vilevile shirika la SIDO Mkoa wa Ruvuma limeweka malengo kwa kushirikiana na wananchi na halmashuri za wilaya zote za mkoa kuhakikisha kunakuwepo maeneo maalum kwa ajili ya shughuli za viwanda vidogo kila wilaya.
MIRADI MBALIMBALI
Pia shirika linasimamia mradi wa Muunganisho wa Ujasiriamali Vijijini (MUVI) unaofadhiliwa na Ifad, unaolenga kusaidia kuongeza thamani kwa mazao ya alizeti na mhogo, kwa wilaya za Namtumbo, Songea na Mbinga. Mradi unasimamia vikundi 14 katika vijiji 14 vyenye wanachama 397.
Mpaka sasa mradi umesaidia vijiji vinane kukamilisha ufungaji wa mashine za kukamua mafuta ya alizeti, hivyo kutoa fursa kwa wananchi kuongeza uzalishaji wa alizeti ili kukidhi mahitaji ya soko.
Ndedya anasema mradi unalenga kupunguza uuzaji wa mazao yakiwa ghafi, kwa kuhamasisha uongezaji thamani , lakini pia mradi utasaidia katika upatikanaji wa taarifa za masoko kwa mazao yote.
“Pia kuunganisha wadau muhimu katika kuongeza thamani kwa mazao husika, ili kilimo kiwezo kuleta tija kwa wakulima wa vijijini na kuongeza kipato na hatimaye kupunguza umasikini,”anasema.