Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Msaada wa Sheria kwa Wanawake na Watoto (WLAC), Theodosia Muhulo Nshala, akizungumza na wanahabari katika kongamano hilo.
Mmoja wa washiriki wa kongamano hilo, Kuruthum Dindili (katikati), akizungumza na wanahabari katika kongamano hilo.
Kongamano likiendelea.
Kongamano likiendelea.
|
Na Dotto Mwaibale
WALEMAVU wenye mahitaji maalum wameonekana kusahaulika na serikali kwa kuwawezesha kufikia haki zao kama mchakato wa kupiga kura kutokana na kukosekana kwa miundombinu rafiki.
Kauli hiyo imetolewa Dar es Salaam leo asubuhi na Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Msaada wa Sheria kwa Wanawake na Watoto (WLAC), Theodosia Muhulo wakati wa mafunzo kwa wanawake walemavu wenye mahitaji maalum kuelekea uchaguzi.
Lengo ikiwa ni ushiriki wa wanawake wenye mahitaji maalum katika kushiriki na kujitokeza katika mchakato wa uchaguzi mkuu unaotarajia kufanyika Oktoba 25,mwaka huu pamoja na kujenga na kukuza uelewa.
“Kundi hili limesahaulika kwa serikali yetu hivyo kwa kuwapa semina hii kunawafanya wasionekane kutengwa na jamii ndiyo maana tumeona tuwaite na kuwaongezea uelewa wao katika kushiriki uchaguzi mkuu ikiwa ni pamoja na kushiriki, kuchagua na kuchaguliwa,” alisema.
Alisema serikali inapaswa kujua mahitaji ya walemavu kwenye michakato ya jamii,kwani hakuna sehemu maalum ya watu wa kundi hilo kwa kuwawekea miundombinu kama sehemu zenye ngazi ili kuweza kufika bila tatizo lolote.
Muhulo alisema wanawake wanapaswa wajitokeze kupiga kura ili waweze kuchagua na kuchaguliwa kwa kumshagua rais, wabunge na diwani ili waweze kuletewa maendeleo na mabadiliko katika jamii zao na si kubaki nyuma.
Kwa upande wake Mbunge wa viti Maalum kupitia Umoja wa Wazazi nchini wa Chama cha Mapinduzi,Kuruthumu Dindili, alimpongeza rais Kikwete anayemaliza muda wake kwa kuwa ni mpenzi wa watu lakini walikosa wa kuwawakilisha bungeni kwani anaamini wangefaidika.
“Kwa bunge lilikopita hatukuwa na mwakilishi bungeni wa kuweza kutusemea malalamiko yetu hasa kwa watu wenye ulemavu wa viungo kwa maana wangekuwepo tungefaidika na mambo mengi sana, walikuwa wamekaa tu kimya bungeni wenzetu wananufaika wao…sisi walemavu hakuna tuanachokipata kupitia wao ndio maana tumeona tuingie na sisi kwenye mchakato,” alisema.
Alisema wanapojitoa kugombea nafasi mbalimbali za kiuongozi wanaonekana ni kichekesho kwa wale wasiokuwa walemavu na kuwabeza kwa kukosa fedha za kufanyia kampeni, aliitaka serikali kwa kutoa nafasi nyingi za wawakilishi walemavu katika bunge lijalo ili kuwe na sauti nyingi za kuleta maendekeo ya kupata mahitaji ya kimsingi kuanzia ngazi za afya, elimu.
Aidha semina hiyo ilihudhuliwa na Chama cha walemavu wa viungo (Chawata), Chama cha Walemavu wa Ngozi (Tas), Chama cha Wasioona (TLD), Chama cha Viziwi Wasioona (Tasodep), Chama cha wazazi wenye watoto wenye vichwa vikubwa na mgongo wazi (Asbat) pamoja na Chama cha Afya na Akili (Tuspo).