Wizara Yawaita Wadau Kushiriki Tamasha la Sanaa na Utamaduni Afrika Mashariki

Dk. Harrison Mwakyembe.

 

WIZARA ya Habari Utamaduni Sanaa na Michezo ambayo ni msimamizi wa sekta ya Sanaa na Utamaduni inawajulisha wadau wake kushiriki katika Tamasha la Sanaa na Utamaduni la Jumuiya ya Afrika Mashariki (JAMAFEST) linalotarajia kufanyika kuanzia tarehe 7 hadi 15 Septemba mwaka huu nchini Uganda.

Tamasha hilo lenye kauli mbiu “TASNIA YA UBUNIFU NA UTAMADUNI NI INJINI YA KUJENGA UMOJA NA KUZALISHA AJIRA” litahusisha nchi wanachama ambapo kila nchi itapaswa kupeleka washiriki wasiopungua mia mbili (200) ambao watahusika katika maonesho mbalimbali yakiwemo burudani mbalimbali, maonesho ya kazi za ubunifu, warsha, mikutano,midahalo,maonesho mbalimbali ya Utamaduni na Sanaa, maonesho ya biashara, michezo ya watoto katika fani mbalimbali, michezo ya jadi, maonesho ya filamu, maonesho ya mavazi na urembo pamoja na maonesho ya vyakula vya asili.

Washiriki wote wanapaswa kuwa na bima ya afya na watatakiwa kujigharamia usafiri wa kwenda na kurudi, pamoja na gharama za malazi na chakula kwa kipindi chote watakachokuwa mjini Kampala.

Aidha Wizara inatoa rai kwa wadau wote wa Sanaa na Utamaduni ambao watapenda kushiriki katika Tamasha hilo kuwasiliana na watendaji wa wizara kwa ajili ya kufanya taratibu za ushiriki wao.

Wadau mnaombwa kuwasiliana na watendaji wa Idara ya Maendeleo ya Sanaa mapema kwa ajili ya taratibu za ushiriki kwa kupiga simu namba 0715531193 au 0784364206 ama kwa barua pepe joyce.hagu@habari.go.tz. Aidha orodha ya majina ya washiriki itapelekwa Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kabla ya wiki ya mwisho ya mwezi Juni mwaka huu.

Imetolewa na:

Genofeva Matemu
Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini,
Wizara ya Habari Utamaduni Sanaa na Michezo
29/05/2017