Wizara ya Viwanda na Biashara Kufanya Mageuzi Makubwa…!

Ofisa Habari na Mawasiliano wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Nicodemus Thomas Mushi akizungumza na waandishi wa habari leo ukumbi wa habari Maelezo.

Ofisa Habari na Mawasiliano wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Nicodemus Mushi (kushoto) akizungumza na waandishi wa habari juu ya masuala mbalimbali chini ya wizara hiyo. Kulia ni Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Habari Bi. Zamaradi Kawawa.

WIZARA ya Viwanda na Biashara imedhamiria kuendeleza Sekta za Viwanda, Biashara, Masoko na Viwanda Vidogo na Biashara Ndogo licha ya changamoto tunazokutana nazo hasa uhaba wa rasilimali fedha. Nia yetu ni kushirikiana na sekta zinazozalisha mali moja kwa moja, ili tuelekee kwenye uchumi wa viwanda tunapoelekea mwaka 2025.

Tunakusudia kuifanya Sekta ya Viwanda nchini kuendelea kusaidia juhudi za serikali katika kupambana na tatizo la ajira nchini kwa kuajiri idadi kubwa zaidi ya watu hasa Vijana wenye ujuzi katika fani mbali mbali na kuzalisha bidhaa bora kwa kiwango kinachohitajika kwa soko la ndani na nje ya nchi.

Mmoja wa waandishi wa habari akiuliza swali mara baada ya hotuba ya Ofisa Habari na Mawasiliano wa Wizara ya Viwanda na Biashara kwa waandishi wa habari, Nicodemus Mushi


Hapa nirudie kuukumbusha Umma juu ya swali linaloulizwa mara kwa mara kuhusu hali ya viwanda vilivyobinafsishwa. Viwanda vilivyobinafsishwa chini ya Sekta ya Viwanda na Biashara ni 74 na kati yake ni viwanda 17 tu ndivyo havifanyi kazi. Juhudi za kufufua viwanda hivyo zinafanyika chini ya Consolidated Holding Corporation (CHC) iliyoko chini ya Wizara ya Fedha, kwa kuzingatia utaratibu wa urekebishaji wa mashirika ya umma. Hivi sasa, majadiliano yanaendelea kwa kushirikiana na wadau mbalimbali na wamiliki wa viwanda hivyo ili kukubaliana jinsi ya kuvifufua. Ni matarajio ya Wizara kuwa zoezi linaloendelea litakamilika haraka iwezekanavyo ili ufufuaji wa viwanda hivyo uanze.

Tunakusudia pia kuifanya sekta ya Biashara kuwa kiungo nyenzo muhimu ya maendeleo kwa nchi yetu kwa kutumia fursa za kibiashara zilizopo ndani na nje ya nchi, ili kuwanufaisha Watanzania wanaojihusisha na sekta hii na kuipa serikali mapato kupitia kodi na ushuru mbali mbali. Tunakusudia kuendeleza Biashara ya Ndani Ikiwa ni Pamoja na Kujenga Dhana ya Kutumia Bidhaa Zilizozalishwa Tanzania (NUNUA BIDHAA ZA TANZANIA, JENGA TANZANIA) pamoja na kuwalinda Wajasiriamali wa Ndani kwa Kutoingiza Bidhaa Mbalimbali Kutoka Nje ambazo Zinaua Soko la Ndani la Bidhaa na kuhakikisha kuwa, bidhaa zinazoingizwa nchini ni zile tu zilizothibitika kuwa na viwango vya ubora, kazi inayofanywa na Shirika letu la Viwango nchini TBS kwa kushirikiana na Mamlaka nyingine.

Tunakusudia kuendelea kuiimarisha sekta ya Masoko kwa kufanya yafuatayo
• Kuendelea kushirikiana na wadau kuendeleza miundombinu ya masoko nchini;
• Kuendelea kushirikiana na wadau katika kuendeleza Vituo vya Ukaguzi wa Pamoja Mipakani (One Stop Border Post OSBP) ambavyo vimethibitika kuwa na ufanisi mkubwa kwa kuokoa muda na kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara pamoja na kupunguza gharama za kufanya biashara.
• Kuimarisha Kamati za Kufanya Kazi Pamoja Mipakani (Joint Border Committees – JBCs) ili kuboresha mazingira ya kufanya biashara mipakani;
• Kukamilisha marekebisho ya sheria zinazokinzana na uboreshaji wa mazingira ya biashara;
• Kuandaa Sera ya Walaji (consumer policy);
• Kushirikiana na wadau kukamilisha maandalizi ya kuanzisha Soko la Mazao na Bidhaa (Commodity Exchange);
• Kuendeleza mfumo wa stakabadhi za mazao ghalani ili uweze kutumika katika uanzishaji wa Soko la Mazao na Bidhaa;
• Kukusanya, kuchambua, kuhifadhi na kusambaza taarifa za masoko kwa wadau kwa wakati;
• Kuhamasisha matumizi ya fursa za masoko ya mipakani, kikanda na kimataifa; na
• Kutangaza bidhaa za Tanzania katika masoko ya ndani na nje.

Baada ya waandishi wa habari katika mkutano na Ofisa Habari na Mawasiliano wa Wizara ya Viwanda na Biashara kwa waandishi wa habari, Nicodemus Mushi.


Katika Eneo la Viwanda Vidogo na Biashara Ndogo,
• Tunaendelea kuboresha vivutio kwa ajili ya Uwekezaji kwenye Viwanda vitakavyotumia malighafi mbalimbali zilizopo nchini vikiwemo Viwanda vya nguo, ngozi, usindikaji matunda, mbogamboga na usanifu wa Madini ya vito.
• Tunaendelea pia kuendeleza Programu ya Muunganisho wa Ujasiriamali Vijijini kwa kutoa ushauri, mafunzo, mitaji na huduma za kiufundi kwa Wajasiriamali.Tunanaendelea pia na Mkakati wa kutoa Elimu na kuwajengea uwezo wakulima wa kusindika mazao kabla ya kuyauza kama vile usindikaji wa asali, utengenezaji wa mvinyo, utengenezaji wa juisi pamoja na ufungashaji wa bidhaa( kuongeza thamani)
• Tunawatazama Wajasiriamali kama kundi maalum linapewa kipaumbele. Lengo letu ni kuhakikiksha kuwa, sekta hii inaendelea kuwakomboa Watanzania kwa kuwapa ajira, kuwapa kipato na kuwaondolea umasikini. Ndio maana Shirika letu la Sido na Chuo chetu cha Elimu ya biashara wapo pamoja nao wakati wote likiwapa mafunzo,kuwakusanya katika vikundi na kuwapa mbinu za kupata mitaji na namna bora ya kufanya shughuli zao kwa Tija
Tunasisitiza kuwa ili Wajasiriamali hawa waweze kufanikiwa, hawana budi kuongeza ubora wa bidhaa zao, wazingatie matumizi ya vifungashio thatibi, watumie vipimo sahihi kwa maelekezo kutoka Wakala wa Vipimo, wapate alama za ubora kutoka TBS, wapate alama za mistari za utambuzi wa bidhaa kutoka GS1 ili waweze kuvuka masoko ya ndani na kuuza bidhaa hizo hata katika masoko ya kimataifa.

DIRA, DHIMA NA MAJUKUMU YA WIZARA YA
VIWANDA NA BIASHARA

DIRA
Kuwa Taasisi shindani, inayokwenda na wakati katika kujenga mazingira wezeshi ya kibiashara ya ndani na kimataifa katika maendeleo ya Viwanda, Biashara na sekta binafsi ili kuwa na uchumi wa kati unaoongozwa na viwanda ifikapo mwaka 2025.

DHIMA
Kuweka mazingira wezeshi na endelevu kwa ajili ya ukuaji wa viwanda, biashara, masoko na viwanda vidogo na biashara ndogo kupitia sera na mikakati madhubuti, kuwezesha ushiriki wa sekta binafsi, kuendeleza ujasiriamali na kuwezesha kupanuka kwa wigo wa uzalishaji, huduma na masoko ili kuongeza ajira, kipato na kuboresha maisha.

MAJUKUMU YA WIZARA
Wizara ya Viwanda na Biashara ambayo imeundwa kwa Tamko la Serikali Na.494 la tarehe 17 Disemba, 2010, ina majukumu ya kuandaa na kusimamia utekelezaji wa Sera za Maendeleo ya Viwanda, Biashara, Masoko na Viwanda Vidogo na Biashara Ndogo ikijumuisha yafuatayo:-

i) Kuandaa, kuratibu na kupitia sera na mikakati ya Sekta ya Maendeleo ya Viwanda, Biashara, Masoko na Viwanda Vidogo na Biashara Ndogo;
ii) Kufuatilia na kuperemba (M & E) utendaji katika viwanda, biashara, masoko, viwanda vidogo na biashara ndogo na taasisi zinazowezesha maendeleo ya viwanda na biashara;
iii) Kubuni na kuandaa programu za kuendeleza sekta za viwanda, biashara, masoko, viwanda vidogo na biashara ndogo na taasisi zinazowezesha maendeleo ya viwanda na biashara;
iv) Kukusanya, kuchambua na kutathmini na kusambaza na kutathmini taarifa za sekta za viwanda, biashara na masoko;
v) Kukuza na kuhamasisha biashara ya ndani na nje;
vi) Kuimarisha utafiti wa maendeleo ya Sekta ya Viwanda;
vii) Kuimarisha ufanisi wa utendaji wa wafanyakazi wa Wizara na Taasisi zake;
viii) Kuboresha upatikanaji wa huduma za kuendeleza biashara;
ix) Kusimamia utendaji wa taasisi zilizo chini ya Wizara;
x) Kusimamia utekelezaji wa sheria zinazosimamia viwanda, biashara na masoko;
xi) Kuboresha mazingira ya utendaji kazi za sekta binafsi; na
xii) Kutafuta fursa za masoko ya bidhaa za Tanzania.

Imeandaliwa na Nicodemus Thomas Mushi,
Ofisa Habari na Mawasiliano,
Wizara ya Viwanda na Biashara,
Julai 10, 2013