Na Anna Titusi – MAELEZO
VYOMBO vya ulinzi na Usalama nchini Tanzania vimefanikiwa kusimamia ulinzi na usalama wa mipaka ya nchi na kuwawezesha wananchi kutekeleza majukumu yao katika hali ya amani na utulivu.
Kauli hiyo imetolewa leo jijini Dar es Salaam na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Dk. Hussein Mwinyi wakati wa ufunguzi wa sherehe za maadhimisho ya miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania Bara katika viwanja vya Mnazi mmoja jijini Dar es Salaam.
Amesema Tanzania imefanikiwa kwa kiasi kikubwa kukomesha vitendo vinavyosababisha kuwepo kwa uvunjifu wa amani huku akiwapongeza wananchi kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama kudumisha amani, utulivu na mshikamano.
“Nachukua nafasi hii kuwapongeza watanzania wenzangu kwa kudumisha amani, Utulivu na Mshikamano katika kipindi chote cha miaka hamsini tangu tupate uhuru, ni matumaini yangu Amani , Utulivu na Mshikamano huu utaendelezwa kwa maslahi ya taifa” Amesema Dk. Mwinyi.
Kwa Upande wake Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali Davis Mwamunyange amesema kuwa jeshi limekuwa na mchango mkubwa wa usalama tangu uhuru mpaka sasa na kuongeza kuwa uimara wake katika miaka 50 ni jambo la kujivunia.
Amefafanua kuwa Jeshi la ulinzi la wananchi wa Tanzania limeundwa na watanzania kwa ajili ya kulinda na kudumisha uhuru wa Tanzania na kubainisha kuwa JWTZ limetoa mchango katika ujenzi wa miundombinu, utoaji wa huduma za afya, uokoaji wakati wa majanga na ulinzi wa amnai ndani na nje ya Tanzania.
Pia amesema maandalizi ya kuunda jeshi dogo yanaendelea ili kuweza kuchukua vijana kwa ajili ya kulitumikia jeshi na kuongeza kuwa sheria ya kutumikia jeshi kwa vijana haijafutwa.
“Bado tunaendelea na utaratibu wa kuchukua vijana wanaomaliza vyuo kwa ajili ya mafunzo na tutaendelea kuboresha jeshi letu katika hali ya Ulinzi na Usalama katika Afrika Mashariki,” amesema, Jenerali Mwamunyange.
Maadhimisho hayo ya miaka hamsini tangu Tanzania bara ipate uhuru yanaongozwa na na kauli mbiu ya Tumethubutu,tumeweza na tunazidi kusonga mbele,”