Wizara ya Ujenzi Yawapiga Msasa Makandarasi Wanawake

Mratibu wa mafunzo hayo Mhandisi Rehema Myeya (kulia) akimkaribisha mgeni rasmi Bi. Elizabeth Tagora kufungua mafunzo hayo kwa makandarasi wanawake.

Mratibu wa mafunzo hayo Mhandisi Rehema Myeya (kulia) akimkaribisha mgeni rasmi Bi. Elizabeth Tagora kufungua mafunzo hayo kwa makandarasi wanawake.

Washiriki wa mafunzo ya makandarasi wanawake wakifuatilia mjadala wa mafunzo hayo mjini Kibaha mkoani Pwani.

Washiriki wa mafunzo ya makandarasi wanawake wakifuatilia mjadala wa mafunzo hayo mjini Kibaha mkoani Pwani.

MAKANDARASI wanawake nchini wametakiwa kujiendeleza kiuchumi na kitaaluma kila wakati ili wawe na uwezo wa kushindana na makandarasi wengine katika zabuni za miradi mikubwa ya ujenzi hapa nchini.
Mkurugenzi wa Sera na Mipango wa iliyokuwa Wizara ya Ujenzi Bi. Elizabeth Tagora amesema hayo wakati akifungua mafunzo ya siku tano ya makandarasi wanawake yalioanza leo mjini Kibaha mkoani Pwani.
“Mafunzo haya yatawawezesha kufahamu vitu vya msingi wakati wa kujaza zabuni na ununuzi wa kazi za ujenzi na hivyo kuwawezesha kushindana kwa usawa na hata kushinda zabuni na kutekeleza ujenzi wa miradi ya barabara kwa usahihi,” amesema Bi. Tagora.
Mkurugenzi huyo amesema Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano itaendelea kuutekeleza sera mbalimbali zenye lengo la kuongeza ushiriki wa wanawake katika sekta ya ujenzi hapa nchini ili kuwawezesha makandarasi wanawake nchini waweze kupanda na kufikia ngazi za juu za ukandarasi na hivyo kuwa na fursa sawa ya ushindani na wanaume wakati wa kuomba zabuni za miradi ya ujenzi wa barabara.
“Kumbukeni kuunganishwa kwa wizara kunawaongezea fursa ya kuomba miradi mingi zaidi katika sekta ya viwanja vya ndege na maeneo ya bandari nchini kote hivyo ni jukumu lenu kuzingatia mafunzo haya na kuongeza ujasiri wa kuthubutu kuombamiradi mikubwa na kuitekeleza kwa ubora unaotakiwa,” amesisitia Bi. Tagora.
Mkurugenzi huyo wa Sera na Mipango amezungumia umuhimu wa mafunzo hayo kwa makandarasi wanawake na kuwataka kuwa chachu ya kujiendeleza zaidi na kuhakikisha wanakuwa na malengo yanayotekelezeka kila mwaka ili kujitathmini.
Naye mratibu wa mafunzo hayo kutoaka Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Eng. Rehema Myeya amesema tangu kuanzishwa kwa mafunzo ya kuwewezesha makandarasi wanawake kuwa na uwezo wa kujaza zabuni na mikataba ya ujenzi idadi ya makandarasi wanawake nchini imeongezeka ambapo sasa zaidi ya kampuni za makandarasi 200, zinashiriki katika ujenzi wa barabara nchini kote.
Eng. Myeya amesema mafunzo hayo ambayo ni endelevu yatakuwa yakitolewa katika kila kanda ili kuongeza idadi ya makandarasi wanawake na kuchochea hamasa katika kila mkoa na hivyo kukuza uchumi wa wanawake na jamii kwa ujumla.
Makandarasi Wanawake kutoka mikoa ya Dar es Salaam, Tanga, Kilimanjaro, Morogoro na Singida wameshiriki mafunzo hayo yenye lengo la kuwawezesha kujua namna bora ya kujaza zabuni na utekelezaji wa miradi ya barabara kwa kuzingatia mkataba.

IMETOLEWA NA KITENGO CHA HABARI NA MAWASILIANO SERIKALINI WIZARA YA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO.