Na Magreth Kinabo – Maelezo Dodoma
SERIKALI imemfukuza kazi Mkurugenzi wa Wanyamapori, Wizara ya Maliasili na Utalii, Obeid Mbangwa na watumishi wengine wawili wa baada ya kukiuka sheria katika utekelezaji wa majukumu yao na kuchangia kuibuka kwa sakata la usafirishaji wa wanyama kupitia Uwanja wa Ndege wa Kilimanjaro kwenda Quatar.
Akizungumza na waandishi wa habari leo katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi za Bunge mjini Dodoma, Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki, alisema watumishi hao wamefukuzwa kazi , yupo aliyeondolewa madaraka na wengine wamepewa onyo kali.
“Upande wa Wizara tumefanya kila jitihada, lengo likiwa kutomwonea mtu yoyote, lakini pia sheria ichukue mkondo wake. Wizara imefikia uamuzi ufuatao; wafanyakazi watatu wamefukuzwa kazi na tayari wameshapata barua,” alisema Waziri Kagasheki huku akiongeza ushahidi wa suala hilo umekusanywa wa kutosha.
Aliwataja watumishi hao kuwa ni Mkurugenzi wa Wanyampori, Obeid Mbangwa ambaye wakati wa kadhia hiyo alikuwa Mkurugenzi Msaidizi Matumizi ya Wanayamapori, Simon Gwera na Frank Mremi wote wanatoka Ofisi ya Uwindaji wa Kitalii – CITES na Utalii wa Picha Arusha.
Waziri Kagasheki alimtaja mtumishi aliyeondolewa madaraka kuwa kutokana na kutochuku hatua kamilifu za ulinzi ambazo zingeweza kuzuia kutokea kwa tukio la utoroshwaji wa wanyama kuwa ni Bonaventura Midala, ambaye ni Mkurugenzi Msaidizi, Uendelezaji Wanyamapori, wakati wa uhalifu huo alikuwa Mkurugenzi Msaidizi Kuzuia Ujangili.
Alisema wengine wawili ni maofisa Wanyamapori Daraja la II wawili waliotekeleza maelekezo ya wakuu wao wa kazi yaliyokinyume na sheria wamepewa onyokali la maandishi, ambao ni Martha Msemo ambaye ni Ofisa Leseni Ofisi ya Uwindaji wa Kitalii, CITES na Utalii wa Picha Arusha na Anthonia Anthony, Ofisa Leseni Ofisi ya Uwindaji wa Kitalii wa Picha Dar es Salaam.
Mwingine aliyepewa onyokali ni Mkuu wa Kituo cha Uwindaji wa Kitalii, CITES na Utalii wa Picha Arusha, Silvanus Okudo ambaye alishindwa kufuatilia kupata maelekezo ya Mkurugenzi wa Wanyamapori kuhusu mtumishi wake aliyekiuka sheria katika utoaji wa vibali. Aidha alishindwa kupeleka kwa Katibu Mkuu taarifa kuhusu mtumishi huyo ili achukuliwe hatua za kinidhamu.
Alisema wapo maofisa wengine ambao uchunguzi dhidi yao unaendelea, ambao ni Mohamed Madehele, ambaye anatoka katika Ofisi ya Matumizi Endelevu ya Wanyamapori na Mariam Nyallu kutoka Kiuto cha Uwindaji wa Kitalii, CITES na Utalii wa Picha – Arusha.
Waziri Kagasheki aliwataka waandishi wa habari na Watanzania kuendelea kutoa ushirikiano na kufichua mambo mengine katika wizara hiyo.