Wizara ya Kilimo Kutumia 328,134,608,000 Mwaka 2013/14

Zao la alizeti

Na Benedict Liwenga-Maelezo, Dodoma

WIZARA ya Kilimo, Chakula na Ushirika inatarajia kutumia jumla ya sh. 328,134,608,000/- katika mwaka ujao wa fedha (2013/14). Takwimu hizo zimetolewa leo mjini Dodoma na Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Mhandisi Christopher Chiza wakati akiwasilisha Bungeni Makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara hiyo kwa mwaka 2013/14.

Alisema kuwa kati ya fedha hizo, Sh. 247,094,320,000 ni kwa ajili ya Matumizi ya kawaida na Shilingi 81,040,288,000 ni kwa ajili ya Matumizi ya maendeleo. Chiza aliongeza kuwa Sh. 210,175,943,000 ni kwa ajili ya Matumizi Mengine (OC) kwa ajili ya Wizara hiyo .

Aidha ,shilingi 25,602,969,000 ni kwa ajili ya Mishahara (PE) ya Wizara na Shilingi11,315,408,000 ni Mishahara (PE) ya Bodi na Taasisi zote zilizoko chini ya Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika. Kwa upande shughuli za maendeleo, Chiza alisema kuwa Wizara hiyo imetenga kiasi cha shilingi 23,927,000,000 ikiwa ni fedha za ndani na shilingi 57,113, 288,000 ni fedha za Nje.

Wabunge wanatarajia kujadili bajeti ya Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika kwa kipindi cha siku mbili ambapo itahitimishwa kesho. Katika hatua nyingine Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika Mhe. Chiza amesema Serikali inatarajia kufufua Kituo cha Kilimo Anga ili kukiwezesha kuwa na ndege na Wataalam watakaosaidia kudhibiti milipuko ya visumbufu vya mazao hasa Nzige.

Mhe. Chiza amesema kwa kiasi kikubwa Serikali imekuwa ikitegemea huduma ya ndege kukodi kutoka kwenye mashirika ya kikanda ya kudhibiti nzige wekundu na nzige wa jangwani ambazo wakati mwingine hazipatikani wakati zinazohitajika.

Kufuatia hali hiyo amesema Wizara katika mwaka wa fedha 2012/13 imekamilisha viwango vya kiufundi (Technical Specifications) kwa ajili ya kutangaza zabuni ya ununuzi wa ndege moja ya kunyunyuzia viuatilifu.

UDHIBITI WA VISUMBUFU VYA MAZAO

SERIKALI itafufua kituo cha Kilimo Anga kwa kukiwezesha kuwa na ndege na Wataalam ili kujenga uwezo wa Wizara ya Kilimo, Chakula na Masoko kudhibiti milipuko ya visumbufu vya mazao hasa Nzige.

Hayo yameelezwa na Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Mhandisi Christopher Chiza wakati akiwasilisha Bungeni Makadilio ya mapato na matumizi ya Wizara hiyo leo.

Mhe. Chiza amesema kwa kiasi kikubwa Serikali imekuwa ikitegemea huduma ya ndege kutoka kwenye mashirika ya kikanda ya kudhibiti nzige wekundu na nzige wa jangwani ambazo wakati mwingine hazipatikani wakati zinazohitajika hali ambayo husababisha Wizara kutegemea kukodisha ndege kutoka sehemu nyingine.

Amesema Wizara katika mwaka wa fedha 2012/13 imekamilisha viwango vya kiufundi (Technical Specifications) kwa ajili ya kutangaza zabuni ya ununuzi wa ndege moja ya kunyunyuzia viuatilifu.

Aidha, Wizara itaweka utaratibu wa kuingia ubia na makampuni binafsi na taasisi zinazotoa huduma kama hizo ili kukijengea uwezo kituo cha Kilimo Anga.

Wakati huo huo, Wizara ya Kilimo, Ushirika na Chakula ilisambaza lita ,6000 za kiuatilifu cha kudhibiti milipuko ya viwavijeshi katika mikoa ya Rukwa, Katavi, Mbeya, Tabora, Shinyanga, Mwanza, Geita. Dodoma, Morogoro na Tanga kunusuru hekta 16,418 za mazao ya nafaka.