Wizara ya Elimu na Ufundi yaweka mikakati ya kukuza usomaji vitabu

Waziri wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa

Na Mwandishi Wetu

WIZARA ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi imesema imeweka mikakati madhubuti ili kuhakikisha kiwango cha usomaji wa vitabu kinakuwa nchini ikiwa ni pamoja na kuzogeza huduma za elimu kwa wananchi.

Changamoto hiyo imetolewa leo jijini Dar es Salaam na Waziri wa wizara hiyo, Dk. Shukuru Kawambwa alipokuwa akizindua Bodi ya Huduma za Maktaba Tanzania (BOHUMATA) inayojishughulisha na usambazaji wa huduma kwa ajili ya kuendeleza masomo kwa jamii.

Dk. Kawambwa amesema ili kukuza kiwango cha usomaji wa vitabu nchini, wizara imejipanga kupanua vyanzo vya mapato kuongeza vitabu na vifaa anuai vya maktaba na kusambaza huduma karibu na wananchi kwa faida yao na huduma inayoendana na wakati.

Aidha Dk. Kawambwa amebainisha kuwa hivi sasa taifa linahitaji watumishi wengi wa maktaba hali inayosababisha Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kutenga fedha za kutosha kuhakikisha inaboresha utoaji wa huduma za maktaba katika shule za msingi sekondari pamoja na vyuo vikuu.

Amedai ili kufanikisha mpango huo mchango wa Bodi ya Huduma za Maktaba unahitajika kwa kiwango kikubwa, huku akiongeza kuwa Serikali kwa kulitambua hilo itaongeza bajeti kukidhi malengo yanayohitajika ikiwa ni pamoja na kuweka mikakati anuai itakayosaidia upatikanaji wa huduma bora inayokidhi mahitaji.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi (BOHUMATA), Profesa Mathew Luhanga amesema lengo la bodi hiyo ni kurahisisha upatikanaji wa elimu, kuboresha huduma za maktaba, kuendeleza utamaduni, kuchapisha na kuhifadhi nyaraka kwa ajili ya kumbukumbu.

Amesema kutokana na ushirikiano wa halmashauri hadi sasa bodi za maktaba zimeundwa katika mikoa yote ya Tanzania bara ambapo hapo awali ilikuwa kwa mikoa michache tu. na kutoa ushauri pamoja na kuwajengea watu utamaduni wa kujisomea vitabu mara kwa mara.