Na Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
WIZARA ya Afya imeeleza azma yake ya kuhakikisha tatizo la upungufu wa dawa katika hospitali zote za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar linapatiwa ufumbuzi wa haraka kwa muda mfupi ujao. Maelezo hayo yametolewa na uongozi wa Wizara ya Afya katika mkutano kati ya uongozi huo na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, katika kuangalia utekelezaji wa kazi za Wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2012-2013.
Katika mkutano huo uliofanyika Ikulu mjini Zanzibar ambapo pia, Makamu wa Pili wa Rais Balozi Seif Ali Idd alihudhuria, Wizara hiyo ya Afya ilieleza kuwa imeamua kuweka mikakati madhubuti katika kuhakikisha tatizo hilo linapatiwa suluhisho.
Mapema Waziri wa Wizara ya Afya, Juma Duni Haji alieleza jinsi mikutano hiyo kati ya Wizara na Rais ilivyosaidia katika kupanga mipango mbali mbali ya Wizara na kumuhakikishia Rais kuwa watendaji wake wameweza kujifunza vyema kutokana na mikutano hiyo.
Uongozi huo chini ya Waziri wake Juma Duni, ulieleza kuwa mbali ya juhudi hizo pia, imo katika mikakati ya kuhakikisha vifo akina mama na watoto watoto wachanga navyo vinapungua. Uongozi huo ulieleza kuwa asilimia 43 tu ni akina mama wanaojifungulia hospitalini hali ambayo inapelekea kesi nyingi hutokea kwa wale wanaojifungulia nje ya hospitali ambapo pale hali ikiwa mbaya ndipo hukimbilia hospitali
Aidha, uongozi huo ulitoa pongezi kwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa kuwapa eneo la kujenga Bohari kuu ya Madawa huko Maruhubi ambalo limejengwa kisasa likiwa na vifaa vya usalama ambavyo ni vya kisasa.
Ilielezwa kuwa kujengwa kwa Bohario hiyo ya Madawa kutasaidia kwa kiasi kikubwa katika suala zima la uhifadhi wa dawa sanjari na mfumo mzima wa ugawaji wa dawa katika hospitali na vituo vyote vya afya Zanzibar kwa kupitia kupitia mfumo wa sayansi na teknolojia.
Ulieleza kuwa compyuta zitatumika katika shughuli hiyo ambapo tayari hivi sasa baadhi ya vituo zimeshafungwa na matarahjiao ya kukamilika kwa vituo vyote na hospitali nchini ni hapo mwakani.
Katika maelezo ya uongozi wa Wizara hiyo, Bohari hiyo ya kisasa imejegwa kwa mashirikiano ya Washirika wa Maendeleo ambao wameunga mkono juhudi za Serikali kwa asilimia kubwa zikiwemo nchi ya Marekani na Denmark.
Wizara hiyo pamoja na mambo mengineyo yakiwemo kuhusiana na bajeti yake pamoja na vipaumbele na malengo iliyojiwekea pia, ilieleza azma yake ya kukamilisha miradi yake mbali mbali Unguja na Pemba. Pamoja na hayo, uongozi umeeleza azma yake katika kupunguza vifo kwa watu wanaoishi na VVU na Ukimwi kwa silimia 50 ifikapo mwaka 2015 huku ikieleza kuwa unyanyapaa kwa watu hao bado ni tatizo katika jamii.
Pia, kupunguza kiwango cha maambukizo ya VVU miongoni mwa wananwake wajawazito kutoka asilimia 0.6 katika mwaka 2010 hadi kufikia asilimia 0.5 mwaka 2013, ikiwa ni pamoja na kuongeza uwezo wa kutoa huduma za afya. Kwa upande wa Malaria, uongozi huo ulieleza juhudi unazozichukua katika kuhakikisha unapiga vita maradhi hayo ikiwa ni pamoja na kuzifanyia kazi Shehia zote ambazo zinazotoka kesi za maradhi hayo.
Aidha, Wizara hiyo ilieleza juhudi inazozichukua katika kuiimarisha Benki ya Damu huku ikieleza umuhimu wake katika kutoa huduma kwa jamii ikiwa ni pamoja na kupunguza vifo vya akina mama na watoto. Kwa upande wake Dk. Shein, alisema kuwa kukamilika kwa Bohari hiyo kutasaidia kufanya kazi kwa ufanisi zaidi pamoja na kwenda na wakati uliopo na kuondokana na utaratibu uliokuwa ukifanyika kabla ya hatua hizo za maendeleo.
Sambamba na hayo, Dk. Shein alieza haja kwa Wizara hiyo kuendeleza juhudi katika kutoa huduma hiyo muhimu ya afya kwa wananchi huku akipongeza juhudi inazozichukua katika kuhakikisha sekya hiyo inaimariska Unguja na Pemba. Katika maelezo yake, Dk. Shein alieleza kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar itaendelea kuchukua juhudi za makusudi katika kuhakikisha wananchi wake wanapata huduma bora za afya na kusisitiza haja na mashirikiano kwa viongozi na watendaji wa Wizara hiyo.