Wizara ya afya yajipanga kudhibiti maambukizi ya TB

Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Hadji Mponda

Na Catherine Sungura, Masasi

WIZARA ya Afya na Ustawi wa Jamii imeimarisha hatua mbalimbali za kudhibiti maambukizi shirikishi ya kifua kikuu na Ukimwi ikiwa ni pamoja na kuchunguza kila mgonjwa wa kifua kikuu kama ana maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (VVU) katika kila kituo cha afya na hospitali zote nchini.
Hayo yamesema leo na Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii Dk. Hadji Mponda kwenye hotuba yake kwenye Kilele cha maadhimisho ya siku ya kifua kikuu duniani yaliyofanyika wilayani hapa. Dk. Mponda alisema katika kutekeleza hilo wizara yake inafanya uchunguzi, kutoa dawa ya kuzuia kifua kikuu kwa watu wanaoishi na VVU pamoja na dawa za mseto za kutibu kifua kikuu hivyo kupunguza muda wa matibabu kutoka miezi nane hadi sita.
Alisema asilimia 88 ya wagonjwa wote wa kifua kikuu wanapona baada ya kupata matibabu sahii kwa kutumia dawa mseto, kiwango hicho ni zaidi ya lengo la Shirika la Afya Duniani ambalo linataka kila mwanachama kuponyesha angalau asilimia 85 ya wagonjwa wa kifua kikuu, “hivyo sehemu kubwa wagonjwa wa kifua kikuu wanao uhakika wa kupona baada ya kuanza matibabu hata kama pia wana maambukizi ya VVU.
Hata hivyo alisema Wizara imeanza kununua na kusambaza aina mpya ya darubini za Light Emitting Diode (LED) zenye uwezo mkubwa zaidi wa kugundua vimelea vya kifua kikuu katika makohozi, hadi kufikia mwisho wa mwaka jana asilimia 80 ya hospitali zote za wilaya zilipata darubini hizo mpya na ifikapo mwishoni mwa mwaka huu, hospitali zote zikiwemo za mashirika ya kidini zitapatiwa lengo ni kuzipa hospitali zote nchini uwezo mkubwa wa kuchunguza vimelea vya kifua kikuu.
“Ninaomba watoa huduma kuhakikisha kwamba kila mgonjwa wa kifua kikuu anachunguzwa maambukizi ya VVU baada ya kupata ushauri nasaha na hivyo hivyo wenye maambukizi ya VVU wachunguzwe pia ugonjwa wa kifua kikuu na wale wote watakaobainika wana maambukizi shirikishi wapewe matibabu sahii ikiwemo dawa za kupunguza makali ya virusi mapema iwezekanavyo kulingana na mwongozo wa Wizara,” alisisitiza.
Aidha Dk. Mponda alisema kwa kauli mbiu ya mwaka huu ya maadhimisho ya kifua kikuu; “Nitatokomeza kifua kikuu kipindi chote cha uhai wangu” ina lenga watoto ambao ni taifa la kesho wategemee kuishi kwenye ulimwengu ambao hakuna mtu yeyote anaugua kifua kikuu hivyo swala la kutokomeza ugonjwa huu si la Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii peke yake bali ni la kushirikisha sekta zote hapa nchini.
Awali Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Dk. Ernest Kasoyaga alisema ugonjwa wa kifua kikuu bado ni tatizo kubwa mkoani hapo ambapo takwimu zinaonyesha idadi kubwa ya wagonjwa waliogunduliwa na kupatiwa matibabu mwaka 2009 kulikuwa na wagonjwa (1,902) , mwaka 2010 (1,898), mwaka 2011 (1,907).
Katika wiki hii ya maadhimisho kwa siku sita waliendesha zoezi la kuhamasisha na kupima makohozi kwa wananchi wa wilaya ya masasi katika vituo saba, ambapo watu wapatao 602 waliojitokeza katika zoezi hilo wakiwemo wanaume 287 na wanawake 315 kati ya watu hao watu 25 waligundulika kuwa na vimelea vya kifua kikuu idadi hiyo ni sawa na asilimia 3.6.
Alisema ongezeko hilo la wagonjwa linatokana na maambukizo ya VVU ambapo toka oktoba mwaka 2010 hadi Septemba 2011 kati ya wagonjwa wa kifua kikuu 1,647 waliopimwa VVU, wagonjwa 440 sawa na asilimia 27 waligundulika na Virusi vya Ukimwi.