Wizara ya Afya Yaandaa Mpango wa Matibabu kwa Watanzania Wote

Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Seif Rashid

Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Seif Rashid

Na Magreth Kinabo, Dodoma
 
SERIKALI iko katika mchakato kuandaa Mkakati wa Kitaifa wa Ugharamiaji Huduma za Afya kwa wananchi ili kuhakikisha kila Mtanzania anapata huduma za afya za msingi bila vipingamizi vyovyote vya kifedha. Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Seif Rashid wakati wa ufunguzi wa kukusanya maoni ya wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma za Jamii kuhusu mkakati huo uliofanyika kwenye ukumbi wa Dodoma Hoteli.

“Serikali imedhamiria kuboresha utoaji wa huduma za afya, moja ya mkakati wa kufikia malengo haya ni kuwa na mkakati endelevu…ninawaomba ushiriki wenu katika majadailiano haya ili tuweze kutoka na mapendekezo yatakayoleta ustawi katika sekta ya afya na hatimaye afya ya watanzania wote,” alisema Waziri huyo.

Aidha Dk. Radhid alisema licha ya uchangiaji wa huduma za afya kuanza rasmi mwaka 1993, ambapo wananchi walitakiwa kuchangia baadhi ya gharama za afya katika vituo vya kutolea huduma vya umma kupitia Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya, ulianzishwa mwaka 1999 na Mfuko wa Afya ya Jamii ulianza mwaka 2001 na bima binafsi za afya kuaanzishwa.

“Pamoja na jitihada hizo, bado rasilimali ni chache wananchi wanaopata huduma za afya kupitia mifuko mbalimbali ni asilimia  ni asilimia 18 tu ya Watanzania wote,” alisisitiza.

Aliongeza kwamba, mkakati huo unalenga kuongeza idadi ya watu watakaopata huduma za afya kwa kutumia mfumo wa bima ili kuwa hakikishia huduma wanazozihitaji. Aliongeza kuwa hivi sasa gharama za matibabu ya afya zimezidi kukua na zitaendelea kukua kuliko uwezo wa Serikali wa kutumia mapato ya kodi.

Alizitaja baadhi ya sababu za kupanda gharama hizo ni taaluma kubadilika kuwa za kisasa, madadiliko ya magonjwa, kuongezeka kwa magonjwa yasiyo ya kuambukiza na kuongezeka kwa idadi ya watu. Alisema ili kuendana na mabadiliko hayo ni muhimu kuwana angalau hospitali ya rufaa moja kila mkoa, sita za wilaya, vituo vya afya 40 na zahanati 100.

Alisema kutokana na hali bajeti ya kutosha inahitajika kila mwaka na kuwa na njia bora ya kuhakikisha kila Mtanzania anakuwa na mfumo wa bima. Kwa Upande wake Kaimu Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Dk. Donan Mmbando alisema takwimu zinaonesha kuwa asilimia 33 ya Watanzania wanaishi katika hali duni ya umasikini.

Alisema pia takwimu zilizopo zinaonesha kuwa zaidi ya asilimia 80 ya Watanzania hawana uhakika wa kupata huduma za afya kwa sababu ya kutokuwa na mfumo mzuri wa kugharamia huduma za afya hali inayosababisha baadhi ya magonjwa kuwa sugu.