Janeth Mushi, Arusha
WIZARA ya Kilimo Chakula na Ushirika kwa kushirikiana na wafadhili toka nchini Japan imeahidi kuchangia kiasi cha shilingi milioni 300 kwa ajili ya ujenzi wa hosteli kwa ajili ya kulala wakulima wanaotoka katika wilaya mbalimbali katika Kanda ya Kaskazini kwa ajili ya maonesho ya wakulima (Nanenane).
Hayo yalisemwa juzi mjini hapa na Waziri wa Kilimo Chakula na Ushirika, Prof.Jumanne Maghembe alipokuwa akifungua maonesho ya 18 ya wakulima katika Kanda ya Kaskazini yanayoendelea katika viwanja vya Themi, Njiro mkoani hapa.
Waziri Maghembe alisema ili maonesho hayo yaweze kuwa na ufanisi zaidi ni lazima juhudi za makusudi zifanyike, hivyo kuwataka viongozi wa TASO Kanda ya Kaskazini kupeleka ramani ya mchoro wa majengo ya hosteli hiyo ili wizara hiyo kwa kushirikiana na TASO kuweza kujenga hosteli hiyo kwa ajili ya wakulima.
“Sekta ya kilimo imepiga hatua kubwa kwani watanzania milioni 31 wanaitegemea sekta hii ambao ni sawa na asilimia 75 ya Watanzania wote inakuwa kwa asilimia 4.2 ambapo ni sawa na asilimia 7.8 ya ukuaji wa uchumi wa nchi, huku ikizalisha asilimia 38 ya fedha za kigeni ambapo mwaka jana sekta hii imeweza kuliingizia taifa Dola Milioni 556 hivyo kuchangia asilimia 27 ya pato la taifa,” alisema Waziri Maghembe
“Ili taifa liweze kuwa na wananchi wenye pato la kati ni lazima uzalishaji uongezeke ambapo lengo la miaka mitano ijayo la serikali ni kuhakikisha kilimo kinakua na kufikia silimia 6 ambapo pato la taifa litaongezeka kutoka katika sekta hii na kukua kwa asilimia 10,” alisema Waziri.
Aliongeza kuwa ili kilimo kiweze kukua ni lazima wakulima kubadilika na kutumia kilimo cha sayansi na teknolojia ili waweze kupata mazao yenye ubora ambayo yatawawezesha kuwa na soko la uhakika ndani na nje ya nchi sambamba na kuongeza uzalishaji wa mazao yao.
Maghembe aliwasisitiza wakulima hapa nchini kuwekeza katika kilimo na serikali itawasaidia katika upatikanaji wa soko ambao umekuwa ni changamoto kubwa kwa wakulima hapa nchini kutokana na wakulima wengi kutokuwa na masoko ya uhakika.
Akizungumzia hali ya chakula hapa nchini Waziri huyo alisema kuwa katika baadhi ya mikoa hapa nchini inakabiliwa upungufu mkubwa wa chakula ambayo ni Shinyanga, Singida, Mwanza, Mara, Arusha, Dar es Salaam.
“Kutokana na upungufu wa chakula unaoikabili baadhi ya mikoa hapa nchini, mwaka huu tumezuia uuzwaji wa chakula nje ya nchi ili wananchi wetu wasife na njaa ila mwakani tutaweka mikakakati ya uuzwaji wa chakula nje ya nchi yetu kwa kutoa elimu kwa wakulima kuongeza uzalishaji ili kuweza kuongeza pato la taifa,” aliongeza Maghembe