Wimbo Wa Adele Watazamwa Mara Bilioni You Tube

adele

Wimbo wa mwanamuziki Mwingereza Adele umevunja rekodi nyingine kwa kutazamwa mara bilioni moja haraka zaidi katika YouTube.
Video ya wimbo huo, Hello, imetazamwa mara bilioni moja katika YouTube siku 87 pekee baada ya kupakiwa kwenye mtandao huo.

Wimbo huo umeupita wimbo wa Psy kwa jina Gangnam Style ambao ulitazamwa mara bilioni moja siku 158 baada ya kupakiwa. Wimbo huo ulichomolewa studioni Julai 2012.

Albamu ya tatu ya Adele, kwa jina 25, ndiyo iliyokuwa maarufu zaidi mwaka 2015 licha ya hali kwamba ilichomolewa studioni Novemba. YouTube wanasema ni video 17 pekee ambazo zimetazamwa mara bilioni moja kwa sasa.

Adele2

Video hizo ni pamoja na Sugar wa Maroon 5, Lean On wa Major Lazer, Love The Way You Lie wa Eminem, Party Rock wa LMFAO, Counting Stars wa OneRepublic, na Chandelier wa Sia.

Wimbo Baby wa Justin Bieber ulichukua miaka minne kutazamwa mara bilioni moja kwenye YouTube. Kwa nyimbo zilizotolewa mwaka 2013, wimbo uliofikia rekodi ya kutazamwa mara bilioni moja upesi ulikuwa Roar wa Katy Perry uliochukua siku 487.
Mwaka 2014, wimbo wa Taylor Swift kwa jina Blank Space ulitumia siku 238.